Mtazamohalisi

Friday, November 12, 2010

Saudi Arabia yaimarisha ulinzi Mecca

Mecca-Saudi Arabia

Kiasi ya mahujaji wa Kiislamu millioni mbili na nusu wanaanza kumiminika katika mji wa mtakatifu wa Makkah, huko Saudi Arabia, huku ulinzi ukiimarishwa kwenye mji huo ambao umewekwa vifaa vipya vya kisasa, ukiwemo usafiri wa treni kurahisisha zoezi hilo la Hijja.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Saudi Arabia, mwanamfalme Nayef bin Abdul Aziz, amesema hawawezi kulipuuza tishio la kundi la kigaidi la Al-Qaida kushambulia wakati wa Hijja hiyo ya siku tano inayoanza kesho kutwa, Jumapili, ijapokuwa kundi hilo halijawahi kufanya shambulio lolote dhidi ya hijja hapo kabla.
Hapo siku ya Jumatano, waziri huyo wa ndani wa Saudi Arabia alielezea kitisho cha  kundi la Al-Qaida kushambulia, lakini hata hivyo akasema uwezekano ni mdogo wa kufanya hivyo.

Dar-es- Salaam, Tanzania
MAHUJAJI 20 waliokuwa wasafiri kwa ndege ya Shirika la Eggypt na Ethiopia kwenda Hijja Meccah na Madina wamekwama uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere wa Dar es Salaam baada ya kutapeliwa fedha zao. Abiria hao ambao walieleza kuwa walipanga safari hiyo kupitia taasisi ya Taibah ya jijini Dar es Salaam, wamekwama kuondoka baada ya taasisi hiyo kuwakana.
Baadhi ya abiria hao waliozungumza na Mwananchi katika ofisi za Taibah jana walisema walilalamikia kitendo hicho na kukiita cha kikatili kwa kuwa hata fedha zao hawajalipwa. Salma Abedi alisema alilipa Sh5.5 milioni kwa ajili ya safari hiyo kwenda na kurudi, chakula na malazi kwa juma moja.

“Kwa kifupi la kusema sina kwani nikikumbuka jinsi nilivyohangaika kuipata hii safari sitaki kuamini eti leo naambiwa hakuna safari wakati Paspoti ninayo na nilikuwa katika listi ya watu wanaoondoka,”alisema Abedi. “Leo hadi muda huu hawajafungua ofisi inavyoonekana haitofunguliwa hebu niambie huu si utapeli huu.

“Nimetoa dola elfu tatu na mia moja kugharamikia safari hii,nimetokea Kongo na nimelipia katika shirika hili nikitegemea kuondoka na ndege iliyoondoka tangu juzi, lakini cha ajabu nimeambiwa safari hakuna na viongozi siwaoni,”alisema Abdalah Abeidi ambaye ni raia wa Kongo.

“Hapa unaponiona nimekuja tangu Oktoba 25, mwaka huu, nimefikia hotelini ambako mpaka leo hii muda wangu wa kukaa pale umekwisha na sina tena fedha za kulipia na mimi hapa ni mgeni sina ndugu nitaenda wapi?sina la zaidi ninachotaka nipewe fedha zangu tu,”alisema Abeidi. Mwenyekiti wa NGO Mkoa wa Tanga Saida Sharifu ambaye nae ni mmoja wa mahujaji alisema amesikitishwa na kitendo cha Taasisi hiyo kwa kudhulumu haki yake.

“Mimi nilitoka Tanga kwa madhumuni ya kwenda katika Hijja na nililipia fedha katika taasisi hii ya Taibah,kitendo cha wao kukimbia ni kitendo kibaya na kinachoumiza kwani kuna watu walifika hadi uwanja wa ndege ila wakarudishwa wengine hawana fedha, kifupi tumedhalilishwa sana,”alisema Sharifu. Aliiomba serikali kufuatilia taasisi hiyo na kuichukulia hatua kwani ni aibu kubwa kwa taasisi ya dini kufanya jambo kama hilo.


Safari hiyo ya kwenda kuhiji Makka na Madina ilikuwa inagharimu Sh 55 milioni ambayo inajumuisha malazi,chakula na usafiri wa kwenda na kurudi. Mbali na hayo, taasisi hiyo ilitoa hati feki ya kusafiria kwa watu na kusababisha mtu mmoja kuwekwa rumande katika uwanja wa ndege wa kimataifa kwa kukutwa na hati hiyo.

Mweka hazina wa taasisi ya Taibah iliyoandaa safari hiyo, Ali Momba alisema taasisi hiyo haiwatambui mahujaji hao kwa kuwa walilipa fedha zao nje ya ofisi. "Hawa walilipa fedha nje ya ofisi zetu na sisi hatuna majina yao," alisema Momba.
  
Ningependa kuwapa pole kwa usumbufu mahujaji waliopatwa na kadhia hii, na kutoa wito kwa serikali kuchukua hatua muafaka za kudhibiti makampuni ya uwakala wa hijja ili aibu kama hii isijirudie.
Hii si mara ya kwanza kwa mahujaji kujikuta katika usumbufu kama huu ,mwaka 2007 ili wachukua zaidi ya wiki na kuilazimu serikali kuingilia kati .

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...