Mtazamohalisi

Saturday, January 15, 2011

Si Risasi Bali Ni Mawe Tu Yamkimbiza Rais Wa Tunisia

Ni kisa cha kijana msomi,26 mchuuzi wa matunda katika mji wa Sidi Bouzid kuhujumiwa na polisi kwa madai ya kufanya biashara kwa njia isiyo halali na kupelekea kujitoa muhanga kwa kujiwasha moto kupinga hali ya ukosefu wa ajira na malipo madogo ya ujira.

Kujitoa muhanga kwa kijana huyo kulipelekea muamko katika mji wa Sidi Bouzid na kuamsha hisia za uchungu juu ya hali ngumu ya maisha  na ukosefu wa ajira na kupelekea umma wa Tunisia kuamua kuingia barabarani kumtaka Rais wao kujiuzulu.

Rais Zine al Abidine Ben Ali aliitawala Tunisia kidiktekta kwa miaka 23 kwa mapinduzi ya kijeshi bila kumwaga damu huku akiwaweka vizuizini wapinzani wake, kuzuia uhuru wa habari huku akishindwa kukabiliana na tatizo la ajira.

Maandamano  ya tarehe 17/12/2010 yaliandaliwa na Chama cha wafanyakazi cha Tunisia nakuchukua muda wa mwezi mmoja kwa kugharimu maisha ya watu 23 yamepelekea Rais Zine al Abidine Ben Ali kuikimbia nchi na kwenda uhamishoni Saudi Arabia .

Nchi za magharibi ambazo zilikuwa washirika wakubwa wa rais Ali zimebariki mapinduzi hayo na kuyaita hatua ya kuelekea kwenye demokrasia ya kweli huku ufaransa mtawala wa zamani wa nchi hiyo ikikataa kutoa hifadhi ya ukimbizi wa rais Ali na Mkewe.

Monday, January 10, 2011

Jicho La Dunia Na Mustakbali wa Sudan

               Bashir kuchukua madeni yote ya Sudan Kusini

Rais wa Sudan, Omar Hassan al-Bashir amesema kuwa yuko tayari kuchukua madeni yote ya nchi hiyo iwapo eneo la Sudan Kusini litajitangazia uhuru wake baada ya kura ya maoni. Taarifa hiyo imetolewa leo na rais wa zamani wa Marekani, Jimmy Carter alipozungumza na kituo cha televisheni cha CNN.

Iwapo ahadi hiyo itathibitishwa, itakuwa ni ishara muhimu ya mapatano kutoka kwa Rais Bashir na itainua mzigo mkubwa wa fedha za serikali katika eneo la Kusini katika siku za mwanzo za uhuru wake unaotarajiwa. Bwana Carter amesema kuwa amezungumza na Rais Bashir ambaye amesema deni lote lazima lipelekwe Sudan Kaskazini na siyo Kusini.

Wakati hayo yakijiri Wasudan Kusini wameingia katika siku ya pili ya kupiga kura ya maoni ya kuamua iwapo wajitenge na Kaskazini na kuwa taifa huru, zoezi litakaloenda hadi tarehe 15 ya mwezi huu wa Januari. Aidha, kwa upande mwingine, watu zaidi ya 20 wameuawa katika mapigano ya Wasudan wenye asili ya Kiarabu wa kabila la Misseria na jamii ya Ngok Dinka katika eneo lenye mzozo la Abyei.
Chanzo: Dw

Sudan Taifa Kubwa kuliko yote Afrika linaelekea kugawanyika pande mbili kutokana na kura ya maoni inayoendelea Sudan ya Kusini .Angalia video upate picha ni wapi Sudan inaelekea


Gharama za Maisha na Ajira Ni Hatari Kwa watawala

Serikali nyingi zimejikuta katika wakati mgumu kutimiza ahadi kwa wananchi wao hasa masuala mazima ya kupanda gharama za maisha na ajira kwa vijana hasa wale wanaomaliza masomo yao ya elimu ya juu.Kupanda kwa gharama za maisha na ajira kwa vijana imekuwa ni jambo linahatarisha uwepo wa serikali.


Ukiyatizama masuala haya kwa makini utagundua kunamguso kwa kila jamii toka pande zote za dunia ila hutofautiana njia zakuyatatua.

Ninachotaka kufungua macho kwa serikali yetu ya Tanzania ni kutafuta njia mbadala za kujiwezesha kujikwamua toka dimbwi zito la umaskini na kusababisha sauti ya mnyonge kuchoka kuvumilia kuona wakubwa wakiji nafasi .

Inapasa kubadilishana uzoefu toka kwa marafiki zetu wa kimataifa ili kufikia lengo la kumkwamua mnyonge ,hebu  rudisha kumbukumbu za uchaguzi wa mawaka 2010 utagundua ni kutokana na hasira za wananchi ndiyo maana vyama vya upinzani vikapata viti vingi bungeni.

Inasemekana kwa matokeo ya uchaguzi mkuu CCM imeathirika hasa suala zima la posho toka bilioni 1 kwa mwezi hadi milioni 800 na kupelekea chama hicho kuchukua hatua za kurekebisha matumizi ya posho hiyo kwa kufuta posho kwa baadhi ya taasisi zake na watendaji kwenye chama.

Hapa tunapata picha ya kuwa CCM isipokuwa makini 2015 mambo yanaweza kubadilika zaidi ikiwa hatua madhubuti ya kurekebisha maisha ya mtanzania hazitachukuliwa.

Nchi kama ya  Falme ZA Kiarabu(UAE) imetunga sheria kwa ajili ya kupambana na tatizo la ajira, wakati nchi nyengine kama Algeria na Tunisia  hali imekuwa mbaya kwa vijana kuingia mitaani kulazimisha serikali zao kuangalia kupanda kwa gharama za maisha na ukosefu wa ajira.


Anger in Algeria sparks fresh riots
Uploaded by euronews-en. - Up-to-the minute news videos.

Sunday, January 9, 2011

Maaskofu Wamng'oa Naibu Meya Arusha

SIKU moja baada ya Maaskofu wa makanisa ya Kikristo mkoani Arusha kutangaza kutomtambua Meya wa Jiji la Arisha, Naibu Meya wa Jiji hilo, Michael Kivuyo (TLP), ametangaza kujiuzuru wadhifa huo.Akitangaza kujiuzulu wadhifa huo, Kivuyo alisema hawezi kuwasaliti wananchi wa Arusha kwa kuongoza sehemu iliyomwaga damu za watu.


Juzi maaskofu wa makanisa ya Kikristo mkoani Arusha, walitoa tamko la pamoja la kutomtambua Meya wa Jiji la Arusha aliyeteuliwa na CCM na kuweka bayana kwamba hawatampa ushirikiano katika uongozi wake.

Walitoa tamko hilowakati wakilaani hatua ya polisi mkoani Arusha, kutumia nguvu kupita kiasi kuvunja maandamano ya amani ya Chadema na hivyo kusababisha vifo vya watu watatu na kujeruhi wengine zaidi ya 20.
Akisoma tamko la umoja wa viongozi wa dini ya kikristo mkoani Arusha, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Arusha, Josephat Lebulu alisema Jeshi la Polisi ndilo lilikuwa chanzo cha vurugu hizo.

Tamko la maaskofu hao lilitolewa siku moja tu tangu Serikali kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha atoe tamko kwamba vurugu zilizotokea Arusha ni tatizo la kisiasa ambalo pia litapaswa kushughulikiwa kisiasa.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, akiwa na wajumbe wa Secretarieti ya chama chake cha TLP mkoani Aruda ya jana asubuhi, Kivuyo alisema anaungana na Watanzania wengine kulaani polisi kutumia nguvu kupita kiasi kutawanya maandamano ya amani ya Chadema.

"Mimi kama Naibu Meya ambaye nilichaguliwa Desemba 18, mwaka jana natangaza rasmi kujiuzuru kwani siwezi kuwasaliti wananchi wa Arusha kwa kuitumikia nafasi hii....kwani ni ukweli uchaguzi haukuwa halali," alisema Kivuyo.

Hili ni pigo la pili kwa CCM baada ya Diwani wake wa Kata ya Sombetini, Alfonce Mawazo kutangaza kujiondoa katika chama chake Jumatano wiki hii na kujiunga na Chadema akidai kuwa amechoshwa na ukatili wa CCM.

Mawazo ambaye alihamia CCM mapema mwaka juzi akitokea TLP akiwa diwani wa kata hiyo, alisema kwa muda mrefu amekuwa akiunga mkono sera za Chadema na sera binafsi za aliyekuwa mgombea wa urais wa chama hicho, Dk Willibroad Slaa.

"Naomba niwaeleze wazi kuwa hata katika Uchaguzi Mkuu ingawa mimi nilikuwa mgombea wa udiwani wa CCM, nilimchagua Dk Slaa kwa nafasi ya urais," alisema Mawazo katika mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Dk Slaa.

Diwani Kivuyo alieleza kuwa, katika mazingira yaliyopo sasa, Uchaguzi wa Meya Arusha unapaswa kurudiwa ili taratibu zifuatwe na amani irejee katika mji wa Arusha.

"Mimi binafsi kabla ya maandamano ya Chadema, nilikwenda kuonana na Mkuu wa Mkoa Arusha, Isdore Shirima nikamuomba aitishe kikao cha vyama vyote na tuzungumze ili kurejesha amani, lakini hakutekeleza," alisema Kivuyo.

Kivuyo ambaye ni Diwani wa Kata ya Sokoni One, alisema anaungana na Watanzania wengine kulaani mauaji ya kinyama ya polisi na kuwapa pole majeruhi wote na wafiwa.

Jumatano wiki hii vurugu kubwa ziliibuka mkoani Arusha na kusababisha polisi kuua watu watatu na wengine zaidi ya 20 kujeruhiwa wakati wakiwatawanya watu walioshiriki maandamano yaliyoandaliwa na Chadema.

Risasi za moto na mabomu ya machozi vilitumika wakati polisi wakizuia maandamano hayo kutekeleza amri ya Mkuu wa Jeshi hilo, Ispekta Jenerali Saidi Mwema.

IGP Mwema alitoa amri ya kupiga marufuku maandamano hyo jioni ya kuelekea siku iliyopangwa kufanyakia kwa maelezo kuwa taarifa za kiintelijensia zimebaini kwamba kungekuwa na vurugu.

Kufuatia tukio hilo viongozi kadhaa wa Chadema akiwamo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Wilbroad Slaa na wabunge kadhaa walikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa madai ya kukusanyika bila ya kibali.

Katika hatua nyingine, TLP mkoa wa Arusha kimemtaka IGP, Said Mwema na Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha kujiuzuru kutokana na kuagiza polisi kuuwa Raia kwa risasi na kujeruhi wengine.

Mwenyekiti wa TLP mkoa wa Arusha, Leonard Makanzo alisema jana kuwa kitendo cha polisi kuvunja kwa nguvu maandamano ya Chadema na kuwauawa kwa risasi watu watatu na wengine zaidi ya 31 kujeruhiwa hakikubaliki.

"Tunaomba wajiuzuru nafasi zao kwani wameshindwa kufanya kazi ya kulinda raia na mali zao badala yake wanafanya kazi ya kufanya vurugu na kuuwa raia kwa kuwapiga risas," alisema Makazo.

Alisema chama hicho kimeridhia Diwani wake, Kivuyo kujiuzuru nafasi ya Naibu Meya na kutaka uchaguzi urudiwa nakufanyika katika mazingira ya haki , amani huku taratibu kidemokrasia zikifuatwa.

Uchaguzi wa Meya Arusha uliingia dosari baada ya kufanyika bila ya kuhusisaha madiwani wa Chadema, hali ambayo ilisabisha mji wa Arusha kuchafuka kwa vurugu na Mbunge wa jimbo la Arusha Mjini, Godbles Lema kukamatwa na polisi, kupigwa na kukimbizwa hospitali baada ya kuishiwa nguvu.
Chanzo: Mwananchi
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...