Mtazamohalisi

Monday, December 13, 2010

Zitto,Shibuda Waundiwa Kamati


Mbunge wa Kigoma kaskazini, Zitto Kabwe, akijuliwa hali na mbunge
wa Maswa Magharibi, John Shibuda, wakati alipolazwa katika hospitali
ya Agha Khan jijini Dar es salaam

WAKATI Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ikitarajiwa kutoa msimamo wa chama hicho juu ya masuala mbalimbali ikiwemo hali ya kisiasa nchini na ndani ya chama hicho, imeelezwa kuwa Mbunge wa

Kigoma Kaskazini Bw. Zitto Kabwe ametakiwa kujipima mwenyewe kisha ajiuzulu, baada ya kupigiwa kura ya kutokuwa na imani na wabunge wa chama hicho.

Imeelezwa kuwa kura za kutokuwa na imani naye, zilizopigwa wiki iliyopita na wabunge wa CHADEMA katika kikao cha kamati yao, kilichofanyika Mjini Bagamoyo, hakizumwondoa moja kwa moja katika cheo chake cha naibu mkuu wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, bali ilikuwa ni ishara ya kuwa watu anaowaongoza bungeni hawana imani naye tena hivyo kumtaka afikirie mwenyewe kisha achukue uamuzi wa kujiuzulu kabla wabunge hao hawajachukua hatua za kinidhamu juu yake.

Habari kutoka ndani ya chama hicho zimebainisha pia kuwa Kamati Kuu iliyoketi mwisho wa juma katika kikao maalumu, imeunda kamati kwa ajili ya kumshauri Bw. Zitto, baada ya wajumbe kuona kuwa kuna umuhimu wa kumsaidia ushauri nasaha kutokana na mwenendo wake ndani ya chama hicho.Vyanzo mbalimbali vimesema kamati hiyo inajumuisha Profesa Mwesiga Baregu, Dkt. Mkumbo Kitila, Shida Salum na mwanachama mwingine wa chama hicho.

Mbali ya kubainika kwa suala hilo, pia habari kutoka vyanzo mbalimbali vya kuaminika zimeeleza kuwa Kamati Kuu ya CHADEMA, imeunda kamati nyingine kumchunguza Mbunge wa Maswa Magharibi, Bw. John Shibuda, kutokana na tuhuma zilizowasilishwa na kamati ya wabunge, iliyokutana wiki
iliyopita Mjini Bagamoyo.

"Nafikiri hilo la Zitto waandishi wamwelipotosha kwa kiasi kikubwa, mimi ninavyojua walichofanya wabunge wale ni kupiga kura ya kutokuwa na imani naye (Zitto), kisha mwenyewe apime uzito wa uamuzi huo kuwa watu anaowaongoza hawana imani naye, kisha mwenyewe ajiuzulu, kabla wabunge wenyewe hawajachukua hatua za kinidhamu juu yake.

"Hata hivyo uamuzi huo wa kuchukua hatua za kinidhamu ikiwemo hata kumwondoa katika cheo hicho, imo katika mamlaka ya Kamati ya Wabunge wa CHADEMA, yaani Party Caucus, wanayo mamlaka hayo kabisa wakiona kuna haja ya kufanya hivyo, baada ya yeye kushindwa kuchukua hatua yoyote hasa kujiuzulu maana ni kiongozi wao wenyewe, hivyo haihusiani na chombo kingine ndani ya chama."Kumbuka pia kuwa naye ataitwa kama alivyoitwa wengine kuhojiwa juu ya kutotekeleza maamuzi halali ya kikao ya kuingia ukumbini siku ya ufunguzi wa bunge kama

ilivyokuwa imeamuriwa...lakini cheo hajavuliwa, mwenyewe apime kisha ajiuzulu," kilisema moja ya chanzo chetu cha habari.

Chanzo chetu kikiwa na tahadhari ya kutotaka kufafanua masuala mengi, pia kilisema kuwa Kamati Kuu ya CHADEMA imeona kuna umuhimu kukaa na Bw. Zitto kisha apatiwe ushauri juu ya mwenendo wake wa kisiasa akiwa kama mmoja wa viongozi waandamizi wa chama hicho, ambapo mbali ya kuwa ni naibu mkuu wa kambi rasmi ya upinzani bungeni pia ni naibu katibu mkuu wa chama hicho kwa upande wa Tanzania Bara.

Nafasi hiyo ya naibu katibu mkuu bara, inamfanya kuwa mmoja wa watu wawili wanaomsaidia Katibu Mkuu Dkt. Willibrod Slaa, mwingine akiwa ni Hamad Mussa Yusuf, kwa Zanzibar, lakini nafasi ya naibu mkuu wa kambi ya upinzani bungeni, inamfanya kuwa msaidizi wa Mkuu wa Kambi, Bw. Freeman Mbowe.

Kwa upande wa suala la Bw. Shibuda, vyanzo vyetu vilieleza kuwa mbunge huyo ambaye alihamia CHADEMA kutoka Chama Cha Mapinduzi, siku chache kabla ya kampeni za uchaguzi kuanza, baada ya kubwagwa katika kura za maoni, atachunguzwa kwa tuhuma kadhaa, ikiwa ni pamoja na kutotii maagizo na maamuzi kikao halali cha chama, kulaumu na kulalamikia nje ya chama maagizo na maamuzi hayo, kujaribu au kutaka kuleta mgawanyiko ndani ya chama.

"Bw. Shibuda alisema hana kosa wala hana haja ya kuomba msamaha, chanzo hicho kilisema wabunge walikuwa wazi kabisa kwake, wakimwambia asifikiri wanamwogopa, asifikiri kuwa wao hawakushinda uchaguzi...maana amekuwa akijigamba kuwa yeye ametumwa na watu wa Maswa.Juhudi za gazeti hili kuwapata viongozi wa chama hicho kuzungumzia taarifa hizo hazikuzaa matunda jana.

Chanzo: Majira

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...