Mtazamohalisi

Thursday, December 16, 2010

John Tendwa Ataka Katiba Mpya Kabla Mambo Hayajaharibika


Msajili wa vyama vya siasa,John Tendwa
Mwangwi wa kudai katiba mpya umezidi kusikika kila kona ya nchi baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa juzi kuvunja ukimya na kusema kuwa iundwe katiba mpya sasa kabla mambo hayajaharibika. Msajili huyo, ambaye ni mwajiriwa wa Serikali, alionyesha ujasiri mkubwa juzi aliposema bila kutafuna maneno kuwa kinyume na katiba iliyopo sasa, katiba mpya inayotakiwa lazima itokane na mapendekezo ya mkutano wa kitaifa wa kikatiba utakaojumuisha watu wa kada mbalimbali.

Kauli hiyo ya mlezi wa vyama vya siasa nchini ni nzito mno, kwa maana ya kutolewa na mtu mwenye mamlaka ya kusimamia shughuli za vyama vilivyoanzishwa kisheria mwaka 1992 kufanya kazi za siasa zenye lengo la kutoa changamoto kwa chama kilicho madarakani. Kauli kama hiyo inapotolewa na kiongozi wa juu serikalini inaifanya serikali yenyewe ione umuhimu wa kutafakari kwa kina madai ya kuwapo katiba mpya ambayo yametolewa na kada mbalimbali nchini mwetu.

Akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TDC), Tendwa alisema kuwa katiba ya sasa ya Tanzania pamoja na nchi nyingine katika Afrika Mashariki bado zina misingi ya kikoloni na akaongeza kuwa maendeleo yaliyopo katika nchi hizo pengine yangekuwa makubwa zaidi iwapo nchi hizo zingekuwa na katiba zinatokana na matakwa ya wananchi wenyewe.

Msimamo huo wa Msajili unakuja siku chache baada ya viongozi wa ngazi za juu, wakiwamo mawaziri wakuu wastaafu, majaji, wanasheria, vyama vya siasa na wanaharakati kusema kuwa katiba iliyopo sasa haikidhi mahitaji ya sasa, hivyo lazima iandikwe upya kwa kuzingatia matakwa ya wananchi walio wengi.

Msimamo wa kiongozi huyo pia umekuja muda mfupi baada ya Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani kusema kuwa serikali haina fedha za kuandika katiba mpya, hivyo zoezi la kuifanyia marekebisho katiba iliyopo litaendelea kufanyika pale tu unapokuwapo umuhimu wa kufanya hivyo. Alisema wanaodai katiba mpya ni watu wa barabarani ambao alidai hawana uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya katiba na sheria.

Ndio maana tunasema kuwa katika mazingira hayo, kauli ya Tendwa ambaye pia ni mwanasheria na mwajiriwa wa serikali hiyohiyo iliyomwajiri Waziri Kombani, ni nzito kiasi cha kuibua maswali mengi kuhusu iwapo Serikali ya Rais Kikwete na chama chake cha CCM vina msimamo wa pamoja juu ya suala hilo, kwani wengi wanajiuliza hivi sasa iwapo kweli msimamo wa waziri huyo kuhusu kuwapo au kutokuwapo umuhimu wa katiba mpya ni wa chama chake na serikali yake au ni wake binafsi.

Utata kuhusu suala hilo umezidishwa na kauli ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, John Chiligati ambaye aliliambia gazeti dada la The Citizen juzi kuwa chama hicho kiko tayari kukaa na vyama vya upinzani kuzungumzia suala hilo, lakini akaonya kuwa vyama hivyo vipeleke mapendekezo thabiti badala ya kile alichokiita ‘blabla za kisiasa’ alizodai zinafanywa na vyama hivyo hivi sasa.

Sisi tunadhani kuwa kauli hiyo ya Chiligati inathibitisha kuwapo tatizo moja kubwa ndani ya chama chake. Tatizo hilo ni CCM kudhani kuwa katiba iliyopo hivi sasa ni mali yake na yeyote anayezungumzia kuifuta na kuandika mpya ni adui mkubwa anayekitakia chama hicho maangamizi makubwa. Ni dhana itokanayo na kile Jaji Mark Bomani anachokiita woga usio na msingi wa chama hicho kupoteza madaraka.

Ndio maana tunasema kuwa tunahitaji viongozi katika CCM au Serikali yake kama Msajili John Tendwa asaidie kuwafafanulia na kuwatoa hofu viongozi wa chama hicho kwamba katiba iliyopo ni ya wananchi wote na kwamba kuandika katiba mpya itakayokidhi matakwa ya wakati huu kutaepusha utengano na machafuko katika siku za usoni.
Chanzo:  Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...