Mtazamohalisi

Wednesday, December 1, 2010

Ukimwi na Waendao "Dago"

Leo ni siku ya Ukimwi Duniani ili kukumbushana athari ya gonjwa hili katika jamii kwa kushauriana na kuonyesha kujali kwa waathirika wa Ukimwi.Ukimwi umeenea kwa kiasi kikubwa na takwimu zinaonesha kila jamii imepoteza wapendwa wao kutokana na ugonjwa huu na hata kuuguza waathirika.

Ishi kwa matumaini na ukinionesha kidole kimoja vitatu vinakutizama ni kauli mbiu ya wanaharakati wa kupigania haki na kuwatambua waathirika kama sehemu katika jamii yetu na wana haki ya kuishi kama mtu mwengine hadi hapo uhai wake utakapo kwisha.

Ukimwi ni gonjwa ambalo huenezwa kwa njia nyingi lakini leo nimependelea kuangalia ukimwi na waendao "dago". Dago ni kitendo cha wavuvi kutoka sehemu moja kwenda kuweka kambi sehemu nyengine kwa ajili ya kufata mavuno ya samaki. Mara nyingi kambi hiyo haingaliwi muda wala umbali muhimu kinachotizamwa ni muelekeo wa upatikanaji wa samaki(soma kilio cha kina mama juu ya waume zao wanapokwenda dago: http://www.mzalendo.net/habari/zanzibar-women-miss-husbands, )

Kutokana na mabadiliko ya maisha na msukumo wa mahitaji ya kibanadamu,jamii imejikuta ikiwa mbali na wapendwa wao kwa sababu nguvu ya uchumi imewatenganisha na kuwapelekea kukubaliana na ugumu huo.Kawaida safari moja huanzisha nyengine na ndilo hilo hupelekea kuweka dhana ya tahadhari kwani ni wengi wetu tumejikuta kusahau tuliyoyaacha kwa ahadi ya nitawakumbuka nitawajali.

Wakati nikiandika haya, takwimu zinaonesha kuwa wengi wa waathirika wa ukimwi wamepata toka kwa wapenzi wao kwa kutokuwa waaminifu. Umbali na muda wa kutokuwa pamoja umepelekea kutovumilia na kufata vishawishi vya hisia za kimwili bila tahadhari na umakini nakujikuta furaha ya muda kupelekea kugharimu maisha ya wana ndoa.

Msisitizo wa serikali ni kwa wachumba kufanya vipimo vya ukimwi kabla ya kufunga ndoa ni mzuri na umezuia maambukizi ya ukimwi kuenea kwa kiasi kikubwa. Lakini mara baada ya kupima kwa ajili ya kufata sheria mara nyingi zoezi hili haliwi endelevu ukizingatia waendao "dago" ni wengi na warudiapo nyuma kwa wapenzi wao hupokewa kwa shangwe na hamu.

Tabaani, siwezi kuamrisha watu kutumia njia za vizuizi kwani jambo hilo lina wataalamu wake na kuna mitizamo yenye kutofautiana kuhusu uhalalishwaji wake na athari yake katika jamii. Unaweza kuona migongano ya fikra mara baada ya kiongozi mkuu wa kanisa katoliki papa benedict vi aliporuhusu utumiaji wa kondomu kwa kupitia link hii: http://www.bbc.co.uk/swahili/habari/2010/11/101120_pope_condoms.shtml

Hivyo basi ,kiushauri na kimtazamo wa kuonesha kujali itakuwa jambo la busara na hekima kama wana ndoa watachukua uamuzi wa kutizama afya zao kwani jambo hili litajenga tabia kwa wana ndoa kuwa waaminifu na hata pia kuzuia maambukizi si tu kwa mpenzi wako bali pia kiumbe kitakachopatikana kutokana na kutocheza salama.

Takwimu za maambukizo ya ukimwi zinaonesha 68% ya watu walioathirika na ukimwi duniani ni kutoka kusini mwa jangwa la sahara . Ili kuweza kushinda vita hivi lazima tukubali kubadilika lazima zoezi la kupima afya liwe endelevu- ahsante.

Video hapo chini inaelezea jinsi watoto wasio na hatia walivyo athirika na janga hili la ukimwi, endelea......

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...