Mtazamohalisi

Monday, December 6, 2010

MAWAZIRI NI WA SMZ SIO WA CUF,CCM - BALOZI SEIF IDDI

• Ataka waache ushabiki, waweke mbele maslahi ya Nchi

Na Mwantanga Ame

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amewatahadharisha Mawaziri walioteuliwa kuziongoza wizara za serikali kutekeleza wajibu wao wakizingatia kuwa ni mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na sio kufanya kazi kama Mawaziri wa vyama vya CCM na CUF.

Balozi Iddi, aliyasema hayo jana alipokuwa akifungua kongamano la kumbukumbu kumuenzi aliyekuwa Mkuu wa kituo cha huduma za Sheria Zanzibar marehemu Profesa Haroub Othman, iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Mjini Zanzibar.

Alisema Zanzibar ina ushabiki mkubwa wa vyama, lakini haitakuwa busara kwa Mawaziri walioteuliwa wakaanza kufanya kazi zao kwa misimamo ya vyama vyao huku wakisahau kuwa wao ni viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na sio CCM wala CUF.

Alisema Mawaziri hao wanatakiwa kuwajibika kwa maslahi ya nchi kwa vile wananchi wamejenga matumaini ya kuhudumiwa kwa kuzingatia kanuni za utawala bora zisizotoa nafasi kwa kiongozi kumuonea mtu kwa rangi yake, dini chama ama kijiji alichotoka.

Makamu huyo alisema mambo hayo ni ya msingi na yanahitaji kuzingatiwa na Mawaziri hao kwani ndio jambo pekee litaloiwezesha serikali ya Umoja wa kitaifa kufanya vizuri na dhana halisi ya kuwatumikia wananchi itaweza kufikiwa.
"Serikali ya Umoja wa kitaifa haishinikizwi na matokeo ya uchaguzi bali huundwa kwa nia njema kuaminiana na kwa ridhaa ya vyama husika kabla ya hata kuelekea kwenye zoezi la uchaguzi, msingi mkubwa ni kuweka mbele maslahi ya Zanzibar kuliko maslahi ya vyama vyetu, kijiji mtu anachotoka au maslahi binafsi”,alisema Makamu huyo.

Akiendelea alifahamisha kuwa mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa iliopo Zanzibar, inawataka Mawaziri waliotoka katika Chama cha CCM na CUF kujenga kuaminiana pamoja na kumuamini Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa vile ndio mfumo waliouchagua kuutumia.

Alisema hivi sasa yapo baadhi ya maoni ya wasomi yanayodai kuwapo kwa muundo huo wa serikali kunaifanya serikali ilale usingizi kwa sababu hakuna upinzani wa kuikosoa serikali jambo ambalo halina ukweli kwani bado Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wenye haki ya kuiohoji serikali.

Alisema lengo la serikali hiyo ni moja ya njia ya kuelekea katika demokrasia, ushirikiano katika kuendesha serikali, kupatikana utulivu wa kisiasa ili kuleta maendeleo ya nchi.

Akizungumzia dhana halisi ya kumbukumbu hiyo, alisema marehemu Profesa Haroub wakati wa uhai wake aliamini kwa dhati, amani, upendo na maendeleo yatakuja tu Zanzibar kama kutakuwa na utawala utaowajumuisha Wazanzibari wote.

Alisema dhana hiyo ya Profesa ilitokana na uzoefu alioupata wakati akisimamia uchaguzi wa kwanza katika mfumo wa vyama vingi alipokiongoza kikundi cha Zanzibar Election Monitoring and Observer Group' (ZEMOG) na ripoti yake kutoa mapendekezo kuwa serikali ya umoja ndio jawabu na kuondoa mivutano ya kisiasa.

"Jambo hili alilihubiri na kulieleza kwa nguvu zake zote kwa sababu aliamini, hivyo ni faraja kuona kwamba mwaka huu ndoto yake hiyo ya siku nyingi imetimia na kweli tayari tumeanza kuona matunda ya serikali ya Umoja wa Kitaifa katika nchi yetu" alisema Balozi Iddi.

Mapema Mwenyekiti wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar, Chris Peter Maina alisema mchango wa Profesa Haroub, wakati wa uhai wake tayari umeweza kuwanufaisha Wazanzibari kwa kupata huduma za sheria kupitia kituo hicho.

Nae mmoja wa Wawakilishi wa familia hiyo akitoa shukrani zao alisema wanaiunga mkono serikali iliopo madarakani kwani itaweza kuwatetea Wazanzibari katika maslahi ya Muungano na kinachohitajika ni kuweka kando ushabiki wa kisiasa.
Kongamano hilo liliwapa fursa washiriki mbali mbali kutoa michango yao juu ya mada ya Serikali ya umoja wa kitaifa iliyowasilishwa na Profesa Issa Shivji, akiwemo Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Fatma Abdul-habib Ferej na Naibu Waziri wa Wizara ya Uhusiano wa Kimataifa Mahadhi Juma Maalim na wasomi, wanasheria viongozi wa vyama na wachambuzi wa mambo ya kisiasa

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...