WATANZANIA wamekuwa na ushauri kwa Rais Jakaya Kikwete kwamba atakapounda Baraza la Mawaziri, azingatie kuwa na baraza dogo, lakini lenye dhamira ya kuwatumikia wananchi likiwa na wachapakazi.
Rais Kikwete ameliona hilo, na katika hotuba yake ya kwanza kwa Mkutano wa Kwanza wa Bunge la 10 jana mjini Dodoma, alisema anakusudia kutekeleza matakwa hayo. Katika hotuba yake hiyo, Rais Kikwete alisema, “katika siku chache zijazo nitaunda Baraza la Mawaziri.
Dhamira yangu ni kwamba tupate Serikali makini, yenye watu waadilifu na wachapakazi hodari. Watu wa karibu kufikika na watu ambao watakuwa karibu nanyi wabunge.”
“Watu ambao wataongoza nchi yetu na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na mipango ya Serikali kwa umahiri mkubwa.
Watu ambao wataondoa urasimu katika Serikali, watakuwa karibu na watu na watashirikiana vizuri na Waheshimiwa Wabunge bila kujali vyama vya siasa wanavyotoka.”
Aliwaomba wabunge wawape ushirikiano ili kwa pamoja kutimiza wajibu kwa wananchi waliowachagua. “Wabaneni kisawasawa panapostahili, wasahihisheni wanapoteleza, lakini pia msiwe wachoyo wa kuwapa sifa wanapofanya vizuri,” alisema Rais Kikwete.
Baada ya uteuzi wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, wananchi wamekuwa na maoni ya kumtaka Rais Kikwete ateue Baraza la Mawaziri dogo, lakini lenye watendaji wanaojali maslahi ya wananchi na waadilifu.
Lakini akionekana kutoa kauli iliyolenga moja kwa moja wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambao walitoka nje mara alipoanza kuhutubia jana, Rais Kikwete alisema wabunge hao hawana wa kumlilia zaidi yake, kwani yeye ndiye Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Watakwenda watarudi, hawana mwingine wa kumlilia kwa yao, isipokuwa Serikali ya CCM ambayo mimi ndiye Rais wake; Dk. Mohammed Gharib Bilal ndiye Makamu wake.
Serikali ambayo Dk. Ali Mohammed Shein ndiye Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad ni Makamu wa Kwanza wa Rais na Balozi Seif Ali Idd ni Makamu wa Pili wa Rais,” alisema Rais Kikwete na kushangiliwa na wabunge.
Wakati akianza hotuba yake, wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), walitoka nje kwa kile ambacho walieleza juzi kuwa hawatambui matokeo yaliyompa ushindi Rais Kikwete.
Wakati Rais Kikwete anaanza kulihutubia Bunge saa 10:35 jioni, wabunge wote wa Chadema walitoka nje ya Ukumbi wa Bunge na kuthibibitisha minong’ono iliyozagaa mjini hapa kuwa hawatahudhuria hotuba na sherehe za rais kutokana na kutomtambua.
Wabunge wa Chadema wapo 46. Wakati wabunge hao wanatoka wabunge, wengine walizomea na kupiga meza zao huku wakisema ‘CCM, CCM.”
“Naomba nimalize kwa kuwahimiza Watanzania wenzangu kwamba sote, mmoja mmoja na kwa umoja wetu, tuamue kwa dhati kukusanya nguvu zetu, akili zetu na maarifa yetu yote, kama ndugu wa Taifa moja, kuifanya Tanzania kuwa nchi bora ya kuishi.
Maisha bora kwa kila Mtanzania yanawezekana. Inawezekana, Timiza Wajibu Wako,” alisema Rais Kikwete na kushangiliwa tena na wabunge. Katika hotuba hiyo, Rais alizungumzia pia kukua na kustawi kwa demokrasia katika miaka mitano iliyopita.
Alisema ni makusudio ya serikali kuona demokrasia inazidi kustawi na raia wanapata fursa ya kutoa maoni kwa uhuru na uhuru wa vyombo vya habari unaheshimiwa.
“Tutaendelea kusaidia na kuliwezesha Bunge na Mabaraza ya Halmashauri kutimiza wajibu wao ipasavyo. Tumefanya hivyo miaka mitano iliyopita, naahidi kuwa tutajitahidi kufanya vizuri zaidi katika miaka mitano ijayo,” alisema Rais Kikwete.
Aidha, aliahidi kuendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa maana ya mishahara, marupurupu, malipo ya uzeeni na mazingira ya kazi.
Kuhusu rushwa, alisema mapambano dhidi ya rushwa katika miaka mitano iliyopita, yalichukua hatua muafaka za kujenga uwezo wa kisheria, kimfumo na kitaasisi wa kupambana na rushwa nchini.
“Tumetunga sheria mpya kali zaidi na yenye upeo mpana zaidi wa kukabili tatizo hili. Pia tumetunga Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa wakati wa uchaguzi.
Tumeunda chombo kipya cha kuzuia na kupambana na rushwa, Takukuru, chenye mamlaka zaidi kisheria na chenye uwezo mkubwa zaidi wa rasilimali watu na vifaa wa kutekeleza majukumu yake,” alieleza.
“Ni ukweli ulio wazi kuwa katika kipindi hiki tuhuma nyingi zimeibuliwa, kuchunguzwa na kufikishwa mahakamani.
Watuhumiwa wengi zaidi wamepatikana na hatia na kuhukumiwa. Rushwa kubwa zimeshughulikiwa na vigogo wamewajibishwa bila kuonewa muhali.”
Hata hivyo, pamoja na hayo, alikiri bado ipo haja ya kufanya zaidi kwani tatizo la rushwa bado ni kubwa.
“Nimesikia, tumesikia na wamesikia kilio cha wananchi cha kutaka tufanye vizuri zaidi. Tutaongeza bidii katika mapambano haya.
"Naomba wananchi waendelee kutuunga mkono na kututia moyo na hasa Takukuru,” alieleza Rais Kikwete akizungumzia mapambano dhidi ya rushwa.
Aliwashukuru wabia wa maendeleo, nchi na mashirika ya kimataifa kwa misaada yao ambayo imesaidia sana kuifikisha Tanzania hapa ilipo.
Aliwaomba wasichoke na waendelee kuisaidia nchi. Lakini alibainisha kuwa miaka si mingi kutoka sasa, hawatakuwa na ulazima wa kufanya hivyo, kwani mwaka hadi mwaka, nchi imeongeza uwezo wake wa kujitegemea, na ushahidi upo.
Awali, katika hotuba yake, Rais Kikwete alimpongeza Anne Makinda kwa kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge, akisema ni ushindi uliostahili kutokana na historia yake iliyotukuka kwa miaka 35 ya kuwa Mbunge na miaka kadhaa ya utumishi wa umma nchini.
“Ni heshima kwako na fahari kwa nchi yetu na kwamba hatuna ajizi katika kuwapa fursa wanawake. Bila ya shaka tumefungua milango kwa wanawake kuweza kuaminiwa kushika nafasi ya juu zaidi ya uongozi wa nchi yetu, Inshaalah,” alisema Rais Kikwete.
Kwa aliyekuwa Spika wa Bunge hilo, Samuel Sitta alimshukuru na kumpongeza kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kuliongoza Bunge la Tisa, akisema “atakumbukwa kwa mengi mazuri aliyoyafanya katika kipindi chake.”
Kwa wabunge, aliwatakia kila la heri wakati huu wanapojiandaa kuonesha kuwa kweli wamestahili heshima hiyo, lakini akawaasa, “napenda kuwakumbusha kuwa msijisahau kuwatembelea wapiga kura wenu, kwa maelezo mna shughuli nyingi za Bunge na Kamati zake.
“Wananchi hukasirishwa sana wasipowaona wawakilishi wao wakiwatembelea na kuzungumza nao. Aghalabu hasira zao wanazionesha kwenye uchaguzi. Mkumbuke miaka mitano si mingi,” aliwaeleza.
Chanzo:
http://www.habarileo.co.tz/kitaifa/?n=11823