Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad |
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amesema kitendo cha aliyekuwa Kiongozi wa Upinzani Bungeni kutoka chama hicho, Fatma Maghimbi, kuhamia CCM ni haki yake kidemokrasia, lakini hakina athari yoyote kwa chama hicho.
Akizungumza na wandishi wa habari mjini Zanzibar jana , alisema CUF hakijapata athari yoyote kisiasa kwa Maghimbi na aliyekuwa Mjumbe wa mkutano Mkuu wa chama hicho, Juma Othman Juma kuhamia CCM.
“Naweza kusema kwamba hatuoni kama tumepata pigo katika hilo, isipokuwa tunamtakia kila la heri katika maisha yake mapya ya kisiasa”, alisema Katibu Mkuu wa CUF.
Alisema kwamba CUF ipo imara na katika kudhihirisha hilo, majimbo yote 18 kisiwani Pemba yataendelea kushikiliwa na chama hicho cha upinzani.
Maghimbi na mwenzake wamekihama chama cha CUF na kuhamia CCM na walikabidhiwa kadi ya CCM na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kawe jijini Dar es Salaam.
Maalim Seif alisema Maghimbi ambaye alikuwa Mbunge wa Chakechake amekihama CUF baada ya kukosa nafasi ya ubunge kufuatia wanachama kumkataa wakati wa kura ya maoni wakati wa mchakato wa kutafuta wagombea wa chama hicho kisiwani Pemba.
“Wapo watu chama kinakuwa kizuri pale wanapokuwa na madaraka wanapokosa chama kinakuwa kibaya, lakini kuondoka kwao hakutaacha pigo lolote kwa CUF, kwasababu hiki ni chama cha wananchi”, alisema Maalim Seif.
Alieleza kwamba tabia ya viongozi wanaokosa vyeo kuhama vyama sio ngeni, kwa vile wapo waliowahi kufanya vitendo kama vya Maghimbi na wamekiacha chama cha CUF kikizidi kuimarika.
Jijini Dar es Salaa, Naibu Mkurugenzi wa Uenezi na Mahusiano CUF, Ashura Mustapha, alisema Maghimbi hana tena mvuto wa kisiasa.
Alisema mwasisi huyo aliamua kukihama chama cha CUF baada ya kuona hana mvuto tena wa kisiasa.
“Ameamua kuhama kwa sababu anaona amepitwa na wakati na wananchi hawamtaki tena,” alisema.
“Maghimbi anadai eti ameamua kuhama CUF kutokana na Upemba kuzidi katika jimbo hilo, lakini tunaamini kuwa wananchi wenyewe ndio walioamua kufanya mabadiliko baada ya kuona hana mvuto tena wa kisiasa, na hata hivyo pia wanaangalia alama za nyakati upo muda wananchi pia wanahitaji mabadiliko,” alisema Mustapha.
Alisema japokuwa Maghimbi ametumia Demokrasia kuhama chama, lakini pia ameonyesha ni jinsi gani uongozi wake haukua kwa manufaa kwa wananchi.
“Kama kweli Maghimbi hakuwa CUF kwa ajili ya kujinufaisha mwenyewe,asingeweza kuhama kwa kuanguka kipindi kimoja tu,wakati ameongoza kwa miaka kumi,” alisema.