Mwenyekiti wa Chadema,Freeman Mbowe
MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe amesema kuwa ana usongo na CCM na mwaka huu atawapa shida ambayo hawataisahau.
Mbowe alisema hayo jana wakati akizindua tawi na kukabidhi kadi zaidi ya 200 kwa wanachama wapya wa Chuko Kikuu Kishiriki cha Tumaini Tawi la Makumira , mkoani Arusha.
“Kwa kweli nina usongo na CCM, mwaka huu watapata shida sana kwa kuwa hivi karibuni tutafanya zaidi ya operesheni sangara, tutahakikisha tunapita kila kijiji kilichopo Tanzania bara na Visiwani kuwahamaisha watu juu ya dhana nzima ya ukombozi wa nchi hii” alisema Mbowe na kuongeza.
“Jamani CCM ni walaini kuliko embe bovu, pamoja na kutumia polisi na mabomu yao, risasi za moto, usalama wa taifa na rushwa zao lakini hawa tukipambana nao tunawapiga goli 10 asubuhi asubuhi tu,” alisema.
Alisema CCM wasifikiri Chadema wamebweteka na wabunge 48, madiwani wengi na halmashauri wanazoziongoza,hivi sasa ndiyo kazi ya kuchukua madaraka ya nchi imeshaanza kutokana na kuhakikisha kila pembe ya nchi inafikiwa na ujumbe wa ukombozi.
Akiwahutubia kundi la wanachuo wa chuo hicho tawi la Makumira katika Hoteli ya kitalii ya Ndoro nje kidogo ya Jiji la Ausha, alisema wasomi wa vyuo vikuu wakichukua kadi za Chadema bila ya kupiga vita ufisadi na kutetea haki za Watanzania wanyonge ni kazi bure.
“Sisi Chadema tunasema, unatakiwa uhubiri kitu ambacho unakifanya na unachokifanya ndicho unachotakiwa kukihubiri, ndio maana hata ndani ya Chadema tunapiga vita ufisadi na maovu mengine yote yanayofanywa na serikali ya CCM, hata sisi Chadema tunajisafisha wanaofanya vibaya tunawaondoa, hatuoneani aibu,”alisema Mbowe.
Aliwaasa wanavyuo hao kuwa makini na matendo yao na kuongeza kuwa yoyote hata akichakachua kadi za wananchama wa Chadema hatakuwa nafasi ndani ya chama chake.
“Jiungeni kwa wingi tukomboe nchi, kwa taarifa yenu fursa za uongozi Chadema ziko nyingi kwa wasomi kama nyie na chama hiki kinakua kwa kasi sana hapa nchini baaada ya tukio la Januari 5 baada ya serikali kuona kuwa wanaikomesha Chadema kwa kutupiga mabomu na kutuweka ndani,"alisema.
Alisema kila mkoa hivi sasa wanataka kuandamana na kupigwa risasi kama Arusha ili waingie kwenye kumbukumbu ya ukombozi wa Taifa na wameshaanza kuonekana hata jana vyombo vya habari vimeonyesha ya Dodoma na Songea. Mbowe alisema leo baada ya kutoka katika uzinduzi wa tawi hilo ataenda jimboni kwake Hai na baadaye jijini Dar es salam kwenda kupanga mikakati mizito ya kwa ajili kuimarisha chama.
Akigusia kitendo cha polisi siku ya maandamano ya Januari 5, Mbowe alisema viongozi wa Chadema walikuwa tayari kwa lolote hata kupoteza maisha kwa ajili ya kizazi kinachokuja.
“Ndugu zangu ile siku haikuwa ya mchezo, tulianza maandamano yetu pale Hoteli ya Mt. Meru na tulipofika Tangi la maji polisi walifika na bunduki za kivuta na mabomu ya mchozi wakiwa wameshakoki, tukawaambia tupigeni vifuani tuko tayari kufa kwa ajili ya Taifa” Alisema
Naye Mwenyekiti wa muda wa Tawi la Chadema chuoni hapo Mwalimu, Restituta Kayombo akielezea kuwa mwamko wa kuunda tawi chuoni hapo ilikuwa ni changamoto ya uchaguzi wa mwaka jana wakati matokeo yalipokuwa yakitangazwa na kuonyesha Chadema kuongoza katika sehemu nyingi za nchi.
Chanzo:
Mwananchi