KATIBU wa Chama cha Soka Mkoa wa Tanga (TRFA), Salim Kajembe amefariki dunia.
Habari zilizopatikana Dar es Salaam jana na kuthibitishwa na Mwenyekiti wa TRFA, Said Soud ni kuwa Kajembe alifariki jana kwenye hospitali ya Bombo mkoani Tanga kutokana na ugonjwa wa tumbo.
Soud alisema ugonjwa huo ulikuwa ukimsumbua kwa muda mrefu na kuna wakati alienda kutibiwa India, kisha hali yake ikawa nzuri, ingawa siku za karibuni hali ilibadilika tena.
“Ugonjwa wa tumbo ulikuwa unamsumbua kwa muda mrefu, amekuwa akipata nafuu na kuendelea na shughuli zake, ila siku tatu zilizopita hali ilibadilika,” alisema Mwenyekiti huyo.
Alielezea msiba huo kuwa ni pigo kwa wanamichezo mkoani Tanga na Tanzania kwa ujumla, kwani Kajembe ambaye amepata pia kuchezea na kuiongoza timu ya African Sports ya Tanga alikuwa kiongozi mahiri na anayejua majukumu yake.
Alisema marehemu atazikwa leo nyumbani kwake Muheza mkoani Tanga baada ya swala ya Ijumaa.
Kwa mujibu wa Soud, Kajembe aliingia kwenye uongozi wa chama hicho na kukitumikia kwa moyo wote na kuwa miezi ya karibuni aliamua kuandika barua ya kujiuzulu kutokana na sababu za kiafya.
Licha ya kuwa kiongozi wa TRFA, Kajembe ambaye pia amepata kuchezea timu ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ miaka ya nyuma, pia amewahi kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) hadi mwaka 2004.
No comments:
Post a Comment