Mtazamohalisi

Tuesday, November 16, 2010

Wsudani Kusini Waanza kujiandikisha Kura Ya Maoni

Wapiga kura wa Sudan waanza kujiandikisha

Wasudan wanaoishi nchi za nje wanataka vituo vya upigaji kura viongezwe kuanzia Marekani,Uganda, hadi kufikia Australia


Raia wa Sudan kusini hii leo wanaanza kujiandikisha kuwa wapiga kura ili kushiriki katika kura ya maoni Januari 9 mwakani, itakayoamua kama wajitenge na eneo la kaskazini ama waendelee kubakia nchi moja. Zoezi hilo linafanyika siku moja baada ya mkuu wa tume inayoandaa kura hiyo ya maoni kuwanyoshea kidole cha lawama wafadhili wa kigeni kwa kutotuma fedha kwa ajili ya matayarisho ya kura hiyo.
Raia milioni tano wa Sudan wanaombwa kujiandikisha kwenye daftari la wapigaji kura katika zoezi linaloanza leo na kuendelea hadi Desemba mosi mwaka huu. Tume inayosimamia kura hiyo ya maoni imeweka vituo takriban 2,800, vyote vikiwa kusini mwa Sudan, isipokuwa 165. Wasudan wa kusini wanaoishi kaskazini wanaokadiriwa kuwa kati ya 500,000 na milioni mbili, wana haki ya kupiga kura.
Umoja wa Mataifa umesaidia kutoa msaada wa uratibu kwa kusafirisha fomu za kupigia kura katika maeneo mbalimbali ya Sudan, hususan katika maeneo ya vijijini. Huku mchakato wa kuwaandikisha wapigaji kura ukitarajiwa kufanyika vizuri kusini mwa Sudan, hali huenda ikawa ngumu huko kaskazini. Mkurugenzi wa kitengo cha Umoja wa Mataifa kinachohusika na kura za maoni na uchaguzi, Denis Kadima, amesema hawajui kama maafisa watakaowaandikisha wapigaji kura wameelewa walichofundishwa wakati wa mafunzo.
Shirika la kimataifa la uhamiaji, IOM, litasimamia uandikishaji wa Wasudan wanoishi katika nchi za nje,huku vituo vikiekwa katika nchi nane: Australia, Uingereza, Canada, Misri, Ethiopia, Kenya, Uganda na Marekani. Hata hivyo msemaji wa shirika la IOM, George Benjamin amesema uandikishaji wa wapigaji kura utachaleweshwa kwa siku kadhaa nchini Misri, nyumbani kwa jamii kubwa ya Wasudan wanaoishi nje ya Sudan, kwa sababu serikali haijalipa kibali shirika hilo.
Mohammed Ibrahim Khalil, mkuu wa tume inayosimamia maandalizi ya kura ya maoni kuhusu uhuru wa Sudan kusini, amesema zoezi hilo litachelewa pia nchini Marekani na Australia kwa sababu raia wa Sudan kusini wanaoishi huko wametaka kuwekwe vituo zaidi vya kujiandikisha.

Kwa upande mwingine Khalili amesema wafadhili wa kigeni wamekwamisha maandalizi kwa kutotuma fedha kwa waandalizi na kutumia fedha vibaya kwa misaada isiyo na manufaa. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Khartoum hapo jana, Khalil aliikosoa jumuiya ya kimataifa kwa kutotoa fedha moja kwa moja kwa tume inayosimamia kura ya maamuzi kwa mujibu wa sheria.
Serikali ya Sudan imeipa tume hiyo paundi milioni 9 za Sudan na serikali ya Sudan kusini kwa upande wake imetoa paundi milioni 10. Lakini wafadhili wa kimataifa hawaishauri kabisa tume hiyo katika kazi zao nyingi wanazofanya.
Wakati huo huo, kiongozi wa tume ya pamoja ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika, inayolinda amani katika jimbo la Darfur, Ibrahim Gambari, ameonya kwamba hali ya wasiwasi kati ya kaskazini na kusini mwa Sudan huenda ikaenea hadi eneo la magharibi. Gambari amesema UNAMID na tume ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan, UNAMIS, zimeweka mipango maalumu kuzuia kutokea machafuko kati ya kusini na kaskazini kabla kufanyika kura ya maoni Januari 9 mwaka ujao.
Chanzo:Dw Swahili

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...