Mtazamohalisi

Thursday, November 18, 2010

Athari ya Chadema kutomtambua rais

Kwa mara ya kwanza imejitokeza kwa bunge la Jamhuri ya Muungano kupata mshtuko mkubwa baada ya wabunge toka chama cha Chadema kususia hotuba ya rais. Hii imekuja baada ya chama hicho kutoridhishwa na mwenendo mzima wa uchaguzi uliopelekea kutangazwa Rais Jakaya Kikwete wa CCM kuwa mshindi dhidi ya Dk.Wilbrod Slaa wa Chadema na Prof.Ibrahim Lipumba pamoja na vyama vyengine vilivyoshiriki katika uchaguzi.

Chaguzi nyingi zilizopita tumeona chama cha Cuf kikiwa ni chama pekee kuwa na wabunge wengi wa kambi ya upinzani.Kwa kuwa wengi wa wabunge wa Cuf ni kutoka Zanzibar, ili kuleta sura ya muungano Cuf ilishirikiana na vyama vyengine vya upinzani vyenye wabunge kuunda serikali kivuli ya kambi hiyo.

Uchaguzi wa mwaka huu umeleta muamko mkubwa na kupelekea bunge la mwaka huu kuwa na wabunge wengi wa kambi ya upinzani toka Tanzania Bara  kuliko ilivyozoeleka. Ni vyema kukishukuru chama cha Chadema kwani kilio chao dhidi ya ufisadi ,wananchi wamekisikia na kuwakubali. Matarajio hayakuwa kama yalivyopangwa lakini inatia moyo kwa kiasi kikubwa kwa kuiamsha seikali ili kuwajibika kwa kuwatumikia wananchi zaidi.

Kama chama pekee kinachounda serikali kivuli ya kambi ya upinzani, Chadema imekataa kutambua ushindi wa mgombea urais toka CCM .Hii imejidhihirisha jana wakati rais alipokuwa akianza kulihutubia bunge jipya na wabunge wa Chadema kususia nakutoka nje ikiwa ishara ya kutomkubali kuwa rais.

Shaka inakuja  ya kuwa zoezi hili litakuwa endelevu? na nini athari yake ya kutomtambua rais kwani izingatiwe haki za mwananchi ni muhimu hasa suala zima la kuishi kwa amani na utulivu.Sitaki kuangalia juu ya Chadema kama kiongozi wa serikali kivuli ya kambi ya upinzani kwani natumaini wanajua wanahatarisha nguvu ya upinzani bungeni na kupelekea CCM kuendelea kulitawala bunge. Bali ukitizama kwa sura pana utaona wabunge wa Chadema wana wawakilisha wananchi wa majimbo yao na kutokuwajibika kwao kutakuwa ni kuwadhulumu haki zao za msingi.

Uzoefu unaonesha mara nyingi,hali tete kama hii ikitokea inapelekea kuwa na muafaka ili kulinusuru taifa lisijekuingia katika janga na kuhatarisha amani na utulivu. Kabla hatujafikia huko, Chadema ituhakikishie kuwa hatutolifikisha taifa pabaya kwani tuliyoyaona Zanzibar hatutaki kuyaona Tanzania bara.

Kumbuka chaguzi nyingi visiwani ziligubikwa na utata wa uchakachuaji wa kura na kupelekea chama cha Cuf kutomtambua Dk.Salmin Amour 1995 na Dk.Amani Karume 2000 na 2005, na kusababisha uchumi wa visiwa hivyo kuyumba, wananchi kugawanyika na kutoshirikiana katika mambo ya kijamii na pia umwagaji wa damu na huharibifu wa mali za watu.

Jirani zetu wa Kenya wanalosomo ambalo tunaweza kulipitia kwani uchaguzi wao ulipelekea umwagaji wa damu na uharibifu wa mali za watu hadi kufikia jumuiya ya kimataifa kuingilia kati na kufanya muafaka uliounda serikali ya kitaifa.

Napenda kumalizia kwa maneno ya Mh.Seif Sharif Hamad baada ya mauaji ya Tarime kwa kusema"zamani zanzibar ilikuwa inasoma toka Tanzania bara wanavyoishi kwa amani .Na sasa ni muda wa Tanzania bara kujifunza toka Zanzibar".

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...