Mtazamohalisi

Saturday, January 1, 2011

Kikwete: Ni mwaka wa Katiba mpya


Rais Jakaya Kikwete

Rais Jakaya Kikwete ametangaza kuanza mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya. Katika salamu zake za mwaka mpya kwa Taifa jana, Rais Kikwete alisema "...nimeamua kuunda Tume maalum ya Katiba, yaani Constitutional Review Commission. Tume hiyo itakayoongozwa na mwanasheria aliyebobea, itakuwa na wajumbe wanaowakilisha makundi mbalimbali katika jamii yetu kutoka pande zetu mbili za Muungano".

Alisema jukumu la msingi la Tume hiyo litakuwa ni kuongoza na kuratibu mchakato utakaowashirikisha wananchi wote vikiwemo vyama vya siasa, wanasiasa, wafanyabiashara, asasi za kiraia, mashirika ya dini, wanataaluma na makundi mbalimbali ya watu wote, katika kutoa maoni "wayatakayo kuhusu Katiba ya nchi yao".
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, baada ya kukamilisha kukusanya maoni, Tume itatoa mapendekezo yake yatakayofikishwa kwenye vyombo stahiki vya Kikatiba kwa kufanyiwa maamuzi. "Baada ya makubaliano kufikiwa, taifa letu litapata Katiba mpya kwa siku itakayoamuliwa ianze kutumika,"alisema Rais Kikwete.

Rais alisema lengo la kuandikwa kwa Katiba mpya ni kuiwezesha nchi kuwa na Katiba inayoendana na taifa lenye umri wa nusu karne na kwamba mchakato huo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara na kwamba Katiba inayokusudiwa ni ile itakayolipeleka taifa miaka 50 ijayo kwa salama, amani, umoja na kuwepo maendeleo makubwa zaidi.

"La nne ambalo tulilokubaliana kufanya ni kuanzisha mchakato wa kuitazama upya Katiba ya Nchi yetu kwa lengo la kuihuisha ili hatimaye Katiba yetu ya sasa tuliyoachiwa na waasisi wa taifa letu, imeifanyia nchi yetu mambo mengi mazuri na kuifikisha Tanzania na Watanzania hapa tulipo," alisema KIkwete na kuongeza:

".....mwaka 2011, nchi yetu inatimiza miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, miaka 47 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar na miaka 47 ya Muungano wa nchi zetu mbili. Yapo mabadiliko mengi yaliyotokea katika nyanja mbalimbali za maisha ya nchi yetu na watu wake katika kipindi hiki. Kwa ajili hiyo ni vyema kuwa na Katiba inayoendana na mabadiliko na matakwa na hali ya sasa".

Alisema ana matumaini kwamba mchakato huo utaendeshwa kwa amani na utulivu kama ilivyo sifa ya Tanzania na mazoea yetu ya kujadiliana bila kugombana.

"Wananchi watapewa fursa ya kutosha ya kutoa maoni yao kwa uhuru na pawepo kuvumiliana kwa hali ya juu pale watu wanapotufautiana kwa mawazo,"alisema Rais Kikwete na kuonya kuwa pasiwepo kutukanana, kudharauliana, kushutumiana, kubezana, kuzomeana wala kushinikizana.

"Naomba washiriki waongozwe kwa hoja badala ya jazba. Tukiwa na jazba, hasira na kushinikizana kamwe hatutaweza kutengeneza jambo jema. Na inapohusu Katiba ya Nchi itakuwa hasara tupu. Haitakuwa endelevu na kulazimika kufanyiwa marekebisho mengi mwanzoni tu baada ya kutungwa,"alisema.

Alitoa wito kwa Watanzania wenye maoni yao kujiandaa kushiriki kwa ukamilifu katika mchakato huo na kutoa maoni ambayo yatawezesha nchi kuwa na Katiba itakayokidhi matakwa ya sasa na ya miaka 50 ijayo.

Tangazo la Rais Kikwete kuhusu kuanza kwa mchakato wa kuandikwa kwa upya kwa Katiba, ni faraja kwa makundi mbalimbali ya kijamii ambayo tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu, Oktoba 31, 2010 yamekuwa yakitoa wito wa kaundikwa kwa Katiba mpya.

Moto wa kudai katiba mpya, uliwashwa na Chadema Novemba mwaka jana, baada ya kutangaza kutotambua kura zilizomweka madarakani Rais Kikwete. Kutokana na hali hiyo, chama hicho kilianza mchakato wa kushikiza kuundwa kwa katiba mpya kwa kususia hotuba ya Rais Kikwete wakati wa akizindua Bunge la Kumi.

Pia wabunge pamoja na viongozi wa chama hicho walisusia sherehe za kuapishwa kwa Rais. Katika kuendeleza madai hayo, hizi karibuni mbunge wa Jimbo la Ubungo kupitia Chadema John Mnyika aliwasilisha hoja binafsi kwenye Ofisi za Bunge, hoja iliyokuwa na lengo la kudai katiba mpya.

Hivi karibuni pia, CUF walifanya maandamano ya kuwasilisha rasimu ya katiba mpya kwa waziri wa Katiba na Sheria. Pia viongozi mbalimbali wastaafu, walipo madarakani wamekuwa wakieleza umuhimu wa kuwa na Katiba mpya.

Miongoni mwa waliojitokeza adharani na kuunga mkono uwepo wa katiba mpya ni pamoja na Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, mawaziri wakuu wa zamani, Joseph Warioba na Frederick Sumaye , Jaji Mkuu Mstaafu na Agostino Ramadhani, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Jaji Omar Makungu pamoja na waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye aliahidi kumshauri Rais juu ya suala la kuundwa kwa Katiba mpya.

Madai ya Katiba mpya pia yamewahi kutolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa ambaye alisema bayana kuwa katiba mpya iandikwe mapema kabla ya mambo kuwa mabaya, akitoa mfano wa mapungufu ya katiba ya sasa kuwa ni rais kupewa madaraka makubwa.

Lakini akiwa Ikulu kwenye hafla ya kuapishwa Jaji Mkuu Mpya, Mohamed Othman Chande, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Frederick Werema, alisema kuwa haona haja ya kuandikwa katiba mpya badala yake katiba iliyopo, iwekewe viraka.

“Kuandika Katiba mpya hapana, lakini kufanya marekebisho kwa kuondoa au kuongeza mambo fulani kwenye katiba, ruksa,” alisema Jaji Werema.

Wakati huohuo, Rais Kikwete ameutangaza mwaka 2011 kuwa mwaka wa maadhsimisho ya miaka 50 ya Uhuru ambayo kilele chake kitakuwa tarehe 9 Desemba, 2011 ambapo kutafanyika sherehe kubwa na za aina yake nchi nzima na wananchi kushirikishwa kikamilifu.

"Kwa kutambua umuhimu wa aina yake wa maadhimisho ya mwaka huu ya siku ya Uhuru wa Tanzania Bara tarehe 9 Desemba, 2011, tumekubaliana na viongozi wenzangu serikalini kuwa tusherehekee siku hiyo kwa uzito unaostahili," alisema.

Kadhalika Rais alisema jambo jingine ni kufanyika kwa tathmini ya kina ya mafanikio tuliyoyapata na tahmini hizo kuandikwa katika vitabu ili kuhifadhi kumbukumbu hizo muhimu kwa vizazi vijavyo.

"Vitabu na nyaraka hizo vitakuwa kumbukumbu zenye manufaa makubwa kwa wenzetu watakaokuwepo mwaka 2061 wakati wa kusherehekea miaka 100 ya Uhuru wa Tanzania Bara" alisema na kuongeza kuwa pia yatafanyika maonyesho maalum katika Uwanja wa Maonyesho wa Julius Nyerere, Dar es Salaam na kote mikoani kwenye viwanja vya maonyesho, kuelezea mafanikio yaliyopatikana katika nyanja mbalimbali katika miaka 50 tangu Uhuru wa Tanzania Bara.
Angalia video................. JK 2011

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...