Mtazamohalisi

Wednesday, November 24, 2010

Wazungu Wa Unga Kukiona Cha Moto Z'bar


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,
      Maalim Seif Sharif Hamad

VIGOGO wa dawa za kulevya Zanzibar watakabiliwa na hali ngumu, baada ya Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, kumkabidhi jukumu la kudhibiti dawa hizo msaidizi wake, Maalim Seif Sharif Hamad.

Hayo yalibainika jana, baada ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif, kukabidhiwa rasmi ofisi yake katika mtaa wa Migombani mjini Zanzibar na baadaye kuzungumza na waandishi wa habari.

Maalim Seif alisema amekabidhiwa majukumu manne na Dk. Shein ambayo ni mapambano dhidi ya dawa za kulevya, ukimwi, mazingira na kushughulikia kero za walemavu visiwani humo.
Hatua ya Dk. Shein kumkabidhi majukumu hayo msaidizi wake ni kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar Ibara ya 20 ambayo imebainisha wadhifa wa Makamu wa Kwanza kuwa ni mshauri mkuu wa Rais na atatekeleza majukumu atakayopangiwa.
“Suala la dawa za kulevya ni tatizo katika nchi yetu, hivi karibuni imeripotiwa kukamatwa watu wanaojihusisha huko Tanzania Bara na Zanzibar,” alisema Maalim Seif.

Hatua ya Dk. Shein kumkabidhi jukumu hilo Seif, imekuja huku wananchi wengi wakiwemo viongozi wa serikali za mitaa (Masheha) kulalamikia udhibiti finyu wa dawa za kulevya kuwa mgumu kwa sababu hata wanapowaripoti wahusika hawakamatwi.

Alisema, katika kutekeleza majukumu yake suala la mazingira atalisimamia kwa karibu, kutokana na ukweli kwamba eneo hilo ni muhimu kwa maisha ya binadamu na viumbe wengine.
Alisisitiza kuwa uharibifu wa maziungira ni ajenda kuu duniani na Zanzibar itatoa kipaumbele katika suala la kudhibiti uchafuzi wa mazingira

Aidha, alisema serikali ya awamu ya saba itafanya kazi kwa karibu katika kusaidia kupunguza kasi ya maambukizi ya ukimwi, ikiwemo kutoa elimu ya kutosha.


Hata hivyo, Maalim Seif, ambaye alijijengea sifa ya uwajibikaji kazini alipokuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar miaka ya 1980, alisema mafanikio ya serikali yatapatikana iwapo kila mtumishi atawajibika ipasavyo.

Alisema ni wajibu wa kila mtumishi kufika kazini mapema na kutekeleza majukumu yake na kuwataka watendaji kuondoa urasimu.

Maalim Seif, alisema atakuwa mtiifu kwa serikali yake na kuhakikisha anafika ofisini saa 1:30 asubuhi huku akisisitiza wafanyakazi wengine kuwahi kufika kazini.
“Kila mmoja ajue tuko hapa kwa ajili ya wananchi, wananchi wetu wanataka huduma bora, taratibu za kazi zifuatwe na viongozi tusimamie majukumu, mambo ya kusumbua wananchi njoo kesho, kesho kutwa yakomeshwe,” alionya Maalim Seif.

Tayari Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd, ambaye kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ibara ya 20 (7) ndiye kiongozi wa shughuli za serikali katika Baraza la Wawakilishi amekabidhiwa ofisi yake katika mtaa wa Vuga mjini Zanzibar.
Katika hafla ya makabidhiano hayo, Balozi Seif Ali Idd aliwahimiza watendaji kuheshimu mipaka ya kazi zao na kujiepusha na vitendo vya ubadhirifu wa mali za umma.
Chanzo: Tanzania Daima, 23 Novemba 2010

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...