Mtazamohalisi

Sunday, January 9, 2011

Maaskofu Wamng'oa Naibu Meya Arusha

SIKU moja baada ya Maaskofu wa makanisa ya Kikristo mkoani Arusha kutangaza kutomtambua Meya wa Jiji la Arisha, Naibu Meya wa Jiji hilo, Michael Kivuyo (TLP), ametangaza kujiuzuru wadhifa huo.Akitangaza kujiuzulu wadhifa huo, Kivuyo alisema hawezi kuwasaliti wananchi wa Arusha kwa kuongoza sehemu iliyomwaga damu za watu.


Juzi maaskofu wa makanisa ya Kikristo mkoani Arusha, walitoa tamko la pamoja la kutomtambua Meya wa Jiji la Arusha aliyeteuliwa na CCM na kuweka bayana kwamba hawatampa ushirikiano katika uongozi wake.

Walitoa tamko hilowakati wakilaani hatua ya polisi mkoani Arusha, kutumia nguvu kupita kiasi kuvunja maandamano ya amani ya Chadema na hivyo kusababisha vifo vya watu watatu na kujeruhi wengine zaidi ya 20.
Akisoma tamko la umoja wa viongozi wa dini ya kikristo mkoani Arusha, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Arusha, Josephat Lebulu alisema Jeshi la Polisi ndilo lilikuwa chanzo cha vurugu hizo.

Tamko la maaskofu hao lilitolewa siku moja tu tangu Serikali kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha atoe tamko kwamba vurugu zilizotokea Arusha ni tatizo la kisiasa ambalo pia litapaswa kushughulikiwa kisiasa.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, akiwa na wajumbe wa Secretarieti ya chama chake cha TLP mkoani Aruda ya jana asubuhi, Kivuyo alisema anaungana na Watanzania wengine kulaani polisi kutumia nguvu kupita kiasi kutawanya maandamano ya amani ya Chadema.

"Mimi kama Naibu Meya ambaye nilichaguliwa Desemba 18, mwaka jana natangaza rasmi kujiuzuru kwani siwezi kuwasaliti wananchi wa Arusha kwa kuitumikia nafasi hii....kwani ni ukweli uchaguzi haukuwa halali," alisema Kivuyo.

Hili ni pigo la pili kwa CCM baada ya Diwani wake wa Kata ya Sombetini, Alfonce Mawazo kutangaza kujiondoa katika chama chake Jumatano wiki hii na kujiunga na Chadema akidai kuwa amechoshwa na ukatili wa CCM.

Mawazo ambaye alihamia CCM mapema mwaka juzi akitokea TLP akiwa diwani wa kata hiyo, alisema kwa muda mrefu amekuwa akiunga mkono sera za Chadema na sera binafsi za aliyekuwa mgombea wa urais wa chama hicho, Dk Willibroad Slaa.

"Naomba niwaeleze wazi kuwa hata katika Uchaguzi Mkuu ingawa mimi nilikuwa mgombea wa udiwani wa CCM, nilimchagua Dk Slaa kwa nafasi ya urais," alisema Mawazo katika mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Dk Slaa.

Diwani Kivuyo alieleza kuwa, katika mazingira yaliyopo sasa, Uchaguzi wa Meya Arusha unapaswa kurudiwa ili taratibu zifuatwe na amani irejee katika mji wa Arusha.

"Mimi binafsi kabla ya maandamano ya Chadema, nilikwenda kuonana na Mkuu wa Mkoa Arusha, Isdore Shirima nikamuomba aitishe kikao cha vyama vyote na tuzungumze ili kurejesha amani, lakini hakutekeleza," alisema Kivuyo.

Kivuyo ambaye ni Diwani wa Kata ya Sokoni One, alisema anaungana na Watanzania wengine kulaani mauaji ya kinyama ya polisi na kuwapa pole majeruhi wote na wafiwa.

Jumatano wiki hii vurugu kubwa ziliibuka mkoani Arusha na kusababisha polisi kuua watu watatu na wengine zaidi ya 20 kujeruhiwa wakati wakiwatawanya watu walioshiriki maandamano yaliyoandaliwa na Chadema.

Risasi za moto na mabomu ya machozi vilitumika wakati polisi wakizuia maandamano hayo kutekeleza amri ya Mkuu wa Jeshi hilo, Ispekta Jenerali Saidi Mwema.

IGP Mwema alitoa amri ya kupiga marufuku maandamano hyo jioni ya kuelekea siku iliyopangwa kufanyakia kwa maelezo kuwa taarifa za kiintelijensia zimebaini kwamba kungekuwa na vurugu.

Kufuatia tukio hilo viongozi kadhaa wa Chadema akiwamo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Wilbroad Slaa na wabunge kadhaa walikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa madai ya kukusanyika bila ya kibali.

Katika hatua nyingine, TLP mkoa wa Arusha kimemtaka IGP, Said Mwema na Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha kujiuzuru kutokana na kuagiza polisi kuuwa Raia kwa risasi na kujeruhi wengine.

Mwenyekiti wa TLP mkoa wa Arusha, Leonard Makanzo alisema jana kuwa kitendo cha polisi kuvunja kwa nguvu maandamano ya Chadema na kuwauawa kwa risasi watu watatu na wengine zaidi ya 31 kujeruhiwa hakikubaliki.

"Tunaomba wajiuzuru nafasi zao kwani wameshindwa kufanya kazi ya kulinda raia na mali zao badala yake wanafanya kazi ya kufanya vurugu na kuuwa raia kwa kuwapiga risas," alisema Makazo.

Alisema chama hicho kimeridhia Diwani wake, Kivuyo kujiuzuru nafasi ya Naibu Meya na kutaka uchaguzi urudiwa nakufanyika katika mazingira ya haki , amani huku taratibu kidemokrasia zikifuatwa.

Uchaguzi wa Meya Arusha uliingia dosari baada ya kufanyika bila ya kuhusisaha madiwani wa Chadema, hali ambayo ilisabisha mji wa Arusha kuchafuka kwa vurugu na Mbunge wa jimbo la Arusha Mjini, Godbles Lema kukamatwa na polisi, kupigwa na kukimbizwa hospitali baada ya kuishiwa nguvu.
Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...