Mtazamohalisi

Friday, December 24, 2010

Ruzuku: CCM milioni 800/-, Chadema 200/-, CUF 117/-


Msajili wa Vyama vya Siasa,John Tendwa
Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, ametangaza viwango vya mgawo wa ruzuku kwa vyama vilivyotimiza sifa, baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, huku kiwango cha mgawo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ilichokuwa ikipata kila mwezi, kikiwa kimeshuka.


Licha ya CCM kuvipita vyama vingine katika viwango vya mgawo uliotangazwa jana na Tendwa, kiwango cha mgawo wake wa ruzuku, kimeshuka kutoka Shilingi bilioni moja ilizokuwa ikipata kila mwezi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kufikia Sh. milioni 800 inazopata hivi sasa.

Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi, ruzuku hiyo hutolewa kwa chama kilichofikisha kuanzia asilimia tano ya kura za urais na kwa uwiano wa wabunge na madiwani, ambao chama ‘kilivuna’ katika uchaguzi huo.

Mbali na CCM, vyama vingine, ambavyo vinapata ruzuku, baadhi vikilingana na vingine vikitofautiana sifa ya kupata ruzuku hiyo, ni Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi, UDP na TLP. Viwango vya mgawo wa ruzuku hiyo, vilitangazwa na Tendwa alipozungumza na NIPASHE katika mahojiano maalum ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana.

Alisema ruzuku hiyo ilianza kutolewa na ofisi yake kwa vyama hivyo, kuanzia Novemba, baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika nchini Oktoba 31, mwaka huu na ule uliofanyika baadaye katika baadhi ya majimbo kukamilisha uchaguzi huo.

“CCM imeshuka kwa ruzuku. Huko nyuma ilikuwa inapata Shilingi bilioni moja, lakini sasa inapata Sh. milioni 818,” alisema Tendwa.

Hata hivyo, alisema ruzuku kwa uwiano wa madiwani, haijaanza kutolewa kwa vile bado hawajapata takwimu za madiwani, ambao kila chama kilipata, katika uchaguzi huo. “Tunasubiri tuweze kuwa na data za madiwani. Hatuwezi kutoa ruzuku za madiwani bila kupata data. Kwa mfano CCM kuna madiwani wamejiuzulu. Kila mgawo (wa ubunge na madiwani) una fungu lake,” alisema Tendwa. Alisema CCM inapata kiwango hicho, kutokana na kupata asilimia 60.40 ya kura za urais katika uchaguzi huo, ambazo ni sawa na Sh. milioni 354 na asilimia 77 ya wabunge (sawa na Sh. milioni 460) kwa mwezi.

Pia alisema licha ya Chama cha Wananchi (CUF) kupata kura katika majimbo mengi ya uchaguzi, kimepata kiwango kidogo cha mgawo wa ruzuku kulinganisha na Chadema. Alisema hali hiyo inatokana na baadhi ya majimbo kiliyovuna wabunge, kama vile ya kisiwani Pemba kuwa na wapigakura wachache waliokiunga mkono katika uchaguzi huo.

“CUF ilipeleka nguvu kubwa Pemba, lakini huwezi kulinganisha na idadi ya wapigakura kama wa Dar es Salaam,” alisema Tendwa.

Kutokana na hali hiyo, alisema CUF sasa inapata Sh. milioni 117.4, kutokana na kupata asilimia 9.80 ya kura za urais (sawa na Sh. milioni 57.9) na asilimia 10 ya wabunge (sawa na Sh. milioni 56). Alisema katika mgawo huo, Chadema inapata Sh. milioni 203.6, kutokana na kupata asilimia 24 ya kura za urais (sawa na Sh. milioni 146) na asilimia 9.62 ya wabunge (sawa na Sh. milioni milioni 56).

Tendwa alisema vyama vya NCCR-Mageuzi, UDP na TLP havipati ruzuku ya urais kwa vile vilipata chini ya asilimia tano ya kura za urais.

Hata hivyo, alisema NCCR-Mageuzi inapata ruzuku ya Sh. milioni 10, kutokana na kupata asilimia 1.08 ya wabunge wakati UDP na TLP alisema vinapata ruzuku ya Sh. milioni 2.4 kutokana na kupata asilimia 0.42 ya kura za ubunge kila kimoja.

Alisema iwapo viwango vya mgawo wa ruzuku ya madiwani itaongezeka kwa chama husika, viwango hivyo navyo pia vitaongezeka.

Kuhusu fomu za gharama za uchaguzi, ambazo wagombea wanatakiwa kujaza, alisema tarehe ya mwisho, ambayo zinatakiwa ziwe zimerejeshwa ofisini kwake, ni Januari 30, mwakani na kwamba, yeyote atakayekiuka ataadhibiwa kwa mujibu wa sheria. “Wanatakiwa waeleze katika hizo fomu walitumia nini, kiasi gani na kutoka wapi. Wathibitishe kwa risiti,” alisema Tendwa.

Akijibu swali kama kuna mgombea yeyote, ambaye hakujaza fomu, alisema hakuna, isipokuwa aliyekuwa mgombea ubunge kupitia TLP Jimbo la Mtama, mkoani Lindi, Ndaka Wolfugang ndiye aliyechelewa kujaza fomu hiyo.

Kutokana na kasoro hiyo, alisema ofisi yake (Msajili) ilimwekea pingamizi Wolfugang, lakini akarudishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwania nafasi hiyo kwa maelezo kwamba, kuchelewa kwake kujaza fomu hiyo, kulitokana na kuwekewa pingamizi na aliyekuwa mgombea kupitia CCM, Bernard Membe, ambalo baadaye lilitupwa.
Chanzo: Nipashe

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...