Mtazamohalisi

Friday, November 26, 2010

Uongozi si Kuula

Na Hafidh Kido
Wiki hii ndugu Rais wa jamhuri ya Tanzania Jakaya Kikwete, ameteua baraza la mawaziri ambao wataongoza wizara mbalimabali kwa miaka mitano ya mwisho katika uongozi wake. Majukumu ya kufuatilia, kusikiliza na kutekeleza sera za serikali na amri za Rais zitakua juu ya mabega ya wanaadamu hawa.

Cha ajabu na kushangaza akili za wenye busara ni habari za salamu za pongezi kwa wateule hawa; bila kufikiri hawastahiki pongezi hizo, badala yake nilitegemea salamu za pole kwa watu hao walioteuliwa na Rais kushikilia nyadhifa ngumu na zenye kuhitaji moyo mkuu wa kujitolea, tena kwa miaka yote mitano bila kujali sikukuu wala mwisho wa wiki, bila kujali wapo ofisini ama nje ya ofisi, bila ya kujali mwenye kuhitaji msaada unamfahamu ama humfahamu.

Maneno mengi yamevuma na kughariki masikio yetu weye kufikiri, lakini ambalo nimelidaka kwa ngoma zagu za masikio na kuendelea kubaki kwenye ubongo wangu wa kutunzia kumbukumbu ni lile neno ‘wameula.’

Naam! neno hilo limekuwa likijirudia mara kwa mara toka vinywani mwa watu kuwa mtu fulai ameula, ameukwaa uwaziri. Ameula nini? Kuenda kufisidi mali ya umma, ama kuonea wenye kudai haki na kulipiza visasi kwa waliowakosea kabla hawajawa na madaraka makubwa kama hayo ya uwaziri.

Hivyo naomba kueleza jamii kuwa unapoteuliwa na Rais kwa nafasi yoyote si kuwa umeula ama umeukwaa bali unakabiliwa na majukumu mazito ya nchi. Pindi unapoapa kuilinda katiba ya nchi yako si jambo dogo hata chembe, labda uwe na moyo mgumu namna gani. Lazima dhamira itakusuta.

Kumbuka utatumika kuenda kuiwakilisha nchi, ukilala muda wowote tegemea kuamshwa ili ukaitumikie nchi, ulapo sikukuu iwe ya kiserikali au ya kidini, tegemea kupigiwa simu ili ukaitumikie nchi yako. Uwapo na familia yako mnakula raha ufukweni ama mnatembea mandari, tegemea kuitwa ukaitumikie nchi; kifupi muda wako mwingi hutoishi kwa amani wala hakuna raharaha.

Na umalizapo miaka mitano ya utawala kama umefanya madudu ujue jamii itakuhukumu kwa ulichowatendea; wala usidhani watakuacha tu hivihivi ule ulichochuma kwa kutumia jasho na unyonge wao.

Hivyo inapaswa kujilinda na kutazama maendeleo zaidi badala ya kujisifia umeukwaa ukigogo, maana kigogo kikishakauka ndipo utakapojua ulikua unaitumikia jamii ama tumbo lako. Wasaka tonge wanakuandama , hivyo usitegemee kulala usigizi wa pono, kazi kwanza.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...