Mtazamohalisi
Monday, December 13, 2010
Raza:Dhambi Ya Ubaguzi Yaitafuna CCM Z'bar
Mfanyabiashara maarufu na kada wa CCM-Zanzibar
Bw.Mohamed Raza
MFANYABIASHARA maarufu na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) visiwani Zanzibar, Bw. Mohamed Raza amekitahadharisha chama hicho kuwa kitatoweka visiwani humo endapo hakitarekebisha mapungufu yaliyojitokeza katika Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba 2010.
Alisema hayo alipokutana na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana wakati akitoa tathmini yake kuwa ushindi wa chama hicho katika uchaguzi huo haukuwa wa kishindo kama walivyotarajia, kwani asilimia 50 na nukta kidogo walizopata ni dalili mbaya.
Alitoa mfano kuwa miaka ya nyuma CCM kilikuwa na majimbo Pemba, sasa hakuna hata moja na pale Zanzibar hivi sasa majimbo manne yamechukuliwa na wapinzani wao na kuongeza kuwa kama chama hakitakuwa wazi kuelezea yaliyojiri, basi Uchaguzi Mkuu ujao wa 2015 kwa upande wa Zanzibar wasishangae majimbo zaidi yakaangukia upinzani kitendo kitakachofanya chama chao kuambulia nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.
"Kwa kuwa Uchaguzi Mkuu ujao hauko mbali, basi ni vyema chama kikakaa chini na kufanya tathmini ya kina na kwa uwazi kikihusisha Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya chama hicho ili kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza", alisisitiza Bw. Raza.
Bw. Raza alionesha kushangazwa na kutoshirikishwa kwa viongozi wastaafu wa Zanzibar katika mchakato mzima wa uchaguzi. Alisema tangu ufunguzi wa kampeni za uchaguzi visiwani humo hadi kumalizika hakuna kiongozi aliyepewa nafasi kuhutubia mikutano hiyo.
Alisema hata kiongozi aliyepangwa katika ratiba kuhutubia moja ya mikutano hiyo, ratiba hiyo ilifutwa na viongozi wenyewe wa CCM bila sababu za msingi.
Aliutaka uongozi wa chama hicho visiwani humo kuwaeleza wanachama wao kwa nini walifanya hivyo na kusisitiza kuwa viongozi wastaafu wana nafasi zao.Akizungumzia usawa, Bw. Raza aliitaka CCM na SMZ kutenda haki kwa viongozi wote wastaafu, kinyume cha hivyo kitakuwa kinatayarisha na kuunda matabaka ya viongozi hao.
Alisema haoni sababu kwa nini kati ya viongozi hao wastaafu wengine wawe na magari ya kuwaongoza na wengine wasiwe nayo; wengine wapewe magari aina ya benz na wengine wasipewe.Alisisitiza kuwa katika CCM hakuna bwana mkubwa wala umaarufu wa mtu, bali chama wanachokitumikia na kusisitiza kwamba asingetaka kuiona Zanzibar yenye matabaka ya wastaafu na ili kuondokana na hilo katiba ya nchi na sheria zifuatwe katika kuteleza usawa huo.
Awali, Bw. Raza alitoa shukrani na pongezi kwa ushindi wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa 2010 na hasa Zanzibar ambako baadaye kuliundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyojumuisha Chama cha Wananchi (CUF).Bw. Raza alisema serikali hiyo isibezwe wala kupuuzwa ili kudumisha hali ya amani na utulivu visiwani humo.
Chanzo: Gazeti la Majira
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment