Mtazamohalisi

Tuesday, December 14, 2010

Maalim Seif: Pelekeni madai yenu Mahakama ya Afrika


Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar
Seif Sharif Hamadi

Watanzania, jumuia za kiraia na mashirika mbalimbali yameaswa kupeleka mashauri yao katika Mahakama ya Afrika inayoshughulika na haki za binadamu iliyoko jijini Arusha, pale wanapohisi kuwa haki zao za kibinadamu zimekiukwa.


Wito huo ulitolewa jana jijini Dar es Salaam na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad, alipokuwa akifungua semina ya uhamasishaji wa jumuia za haki za binadamu nchini, iliyoandaliwa na Mahakama ya Afrika kuhusu haki za binadamu kwa kushirikiana na serikali na Jumuia ya wanasheria nchini (TLS).
Alisema mahakama hiyo inapewa mamlaka na protokali yake, kuipa nguvu Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu ili kulinda haki za watu na za makundi Afrika, kwa kutoa hukumu za kukazia na mamlaka ya kutoa ushauri pale inapoombwa na nchi mwanachama,AU yenyewe,chombo chake au chombo inachokitambua.

“Ndiyo maana nasema raia katika ujumla wao,jumuia za watu na ,makundi mbalimbali yawasilishe mashauri yao katika mahakama hii pale wanapohisi kutotendewa haki na mamlaka yeyote ile”alisema.

Hamad alisema kuwa pamoja na mahakama hiyo kuwa tayari kupokea mashauri toka mwaka 2008,inasikitisha kuona kwamba mpaka sasa imeshapokea shauri moja tu,kitu ambacho hakikubaliki.

Naye Rais wa Mahakama hiyo, Jaji Gerard Niyungeko, aliviasa vyombo vya habari kujikita katika utoaji wa habari zilizo sahihi,kama zilivyo zenye kuhabarisha na zilizotolewa kwa wakati kuhusu matukio na maendeleo ya ulimwengu,kwa kuwa bila ya kufanya hivyo jamii itabaki bila ya kuhabarishwa au ikapata habari zilizopotoshwa.
Chanzo: Nipashe

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...