Rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy amemtaka kiongozi aliyeng'ang'ania madarakani nchini Ivory Coast Laurent Gbagbo aondoke kabla ya mwisho wa wiki, la sivyo atakabiliwa na vikwazo vya Muungano wa Ulaya.
Rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy
Bw.Gbagbo amepinga miito ya Kimataifa ya kung'atuka madarakani kufuatia uchaguzi wa Rais uliomalizika mwezi uliopita.
Yeye pamoja na kiongozi wa upinzani Alassane Ouattara walidai kuwa wameshinda na kuzusha wasiwasi wa uwezekano wa kuzuka mapigano ya nchini.
Wafuasi wa Ouattara wanasema watafanya maandamano mitaani, siku moja baada ya miliyo ya risasi katika mji mkuu Abidjan.
Rais Sarkozy ameonya kwa kusema kuwa majaliwa ya Bw.Gbagbo na mke wake ni jukumu lao kwa sasa. Na ikiwa ifikao mwisho wa wiki hii hawajaachilia hatamu za uongozi wanaoshikilia kinyume cha chaguo la raia wa Ivory Coast, wataorodheshwa jina kwa jina kwenye orodha ya watu waliopigwa marufuku na Muungano wa Ulaya.
Afisa wa ngazi ya juu wa Marekani naye amenukuliwa akisema kuwa Bw.Gbagbo amepewa mda wa kutosha aondoke la sivyo atawekewa vikwazo vya kusafiri na pia vikwazo vya fedha zake.
Afisa ambaye hakutambulishwa amesema kuwa Gbagbo na familia yake wana nyumba kadhaa katika nchi nyingi ambako angeweza kuhamia lakini asipotii masharti haya huenda akapoteza fursa hiyo na nyumba hizo kuwa marufuku kwake.
Mwandishi wa BBC amesema kuwa hili litawashangaza raia wengi wa Ivory Coast ambao hawakujua siri hiyo wakimuona Gbagbo kama mzalendo anayepigania na kuipenda nchi yake bila kuwa na mali nje.
Watu ishirini waliuawa siku ya alhamisi wakati wafuasi wa Bw Ouattara walipojaribu kuandamana wakielekea kituo cha televisheni ya Taifa na kukabiliana na vikosi vinavyomtii Bw.Gbagbo.
Msemaji wa Bw.Gbagbo alisema kuwa waandamanaji 10 na askari 10 wa jeshi waliuawa.
Maofisa wa kambi ya Bw.Ouattara walitaja idadi ya wafu kuwa 30 na zaidi.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeonya kuwa pande zote mbili zitawajibishwa chini ya sheria ya Kimataifa kwa shambulio lolote dhidi ya raia.
Umoja wa Mataifa pamoja na viongozi wa Umoja wa Afrika na nchi za magharibi wamemuunga mkono Bw.Ouattara kama mshindi wa Uchaguzi uliofanywa huko Ivory Coast.
Chanzo: BBC
No comments:
Post a Comment