Mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu - International Criminal Court (ICC) imetaja majina ya Wakenya sita anaowatuhumu kuhusika kupanga vurugu zilizotokea baada ya uchaguzi mkuu nchini humo mwaka 2007.
Ghasia baada ya uchaguzi mkuu Kenya
Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Fedha Uhuru Kenyatta, ni mmoja ya waliotajwa.
Takriban watu 1,200 waliuawa na zaidi ya wengine 500,000 walizihama nyumba zao kufuatia ghasia hizo.
Siku ya Jumatatu Rais Mwai Kibaki, alitangaza serikali itaendesha uchunguzi wake, hatua ambayo wapinzani wake wameiona ni sawa na jaribio la kuzuia watuhumiwa kupelekwa The Hague.
Ghasia hizo zilizuka baada ya wafuasi wa Bw Kibaki, kutuhumiwa walijaribu kuvuruga uchaguzi.
Uhasama huo ulimalizika baada ya Bw Kibaki na mpinzani wake kisiasa Raila Odinga walipokubaliana kuunda serikali ya mseto na Bw Odinga akawa Waziri Mkuu.
Waziri wa Viwanda Henry Kosgey, naye ametajwa na Bw Ocampo.
Waziri wa Elimu aliyesimamishwa William Ruto, Mkuu wa uendeshaji wa Radio Kass FM, Joshua Arap Sang, katibu wa Baraza la Mawaziri Francis Kirimi Muthaura na na Mkuu wa zamani wa jeshi la polisi Mohammed Hussein Ali, nao majina yao yametajwa na Bw Ocampo.
Polisi nchini Kenya wamewekwa katika hali ya hadhari iwapo baada ya kutangazwa majina hayo kunaweza kuibuka ghasia mpya.
Kila mmoja kati ya hao sita, watatumiwa hati ya kuitwa mahakamani, lakini wakigoma au wakijaribu kuingilia uchunguzi, mathalan kuwatisha mashahidi, Bw Ocampo amesema ataomba kibali cha hati ya kuwakamata.
Swali lililopo ni iwapo waliotuhumiwa hao watajisalimisha au watawekewa kinga na wanasiasa na kukwepa mkono wa sheria.
Katika taarifa yake baada ya tangazo hilo la Bw Ocampo, Rais Mwai Kibaki amesema ana matumaini Mahakama hiyo ya Kimataifa, mchakato wake utatimiza wajibu wake kwa maslahi ya taifa la Kenya.
Rais Kibaki amesema, kama taifa ni lazima walenge mahitaji ya taifa ya maridhiano na kusameheana.
Amewahakikishia Wakenya kwamba serikali imeimarisha ulinzi nchi nzima.
Chanzo: BBC
No comments:
Post a Comment