Mtazamohalisi

Monday, January 3, 2011

Tunaelekea Kula Kwa Kushiba Moshi

Muelekeo wa dunia kwa sasa kila mamlaka inalia hali,ukweli hakuna nafuu ila tutarajie kuumizana ili kufikia malengo ya kiutawala na uchumi.

Mwaka 2010 ulikuwa ni mwaka wa serikali za nchi za ulaya kufunga mkanda kwa kubana matumizi ili kukabiliana na anguko la uchumi, msukumo uliopelekea kufanya hivyo ni kuweza kutunisha mfuko wa kulipa madeni yanayo yakabili mataifa hayo.

Sijui kama tushapata picha kuwa mwaka huu mpya 2011 mlango unaelekea kufungwa na nchi zetu changa haja zetu hatuziwezi tunategemea muhisani mwenye funguo.

Kwa taarifa , wahisani wanahaha kuweka serikali zao sawa maana wanajua wananchi waliowaweka wasipotimiziwa haja zao basi kura itakuwa fimbo.

Kesho wakaazi wa Uingereza  wataanza kukamuliwa kwa kulipa kodi ya ongezeko la thamani(VAT) toka 17% hadi 20% ,athari ya ongezeko la kodi ni kupungua mauzo ya bidhaa sokoni nakutokana na hilo Makampuni yatabidi kupunguza wafanyakazi na kuathiri soko la ajira.

 India inakabiliwa na ongezeko la bei ya vyakula,nchi ambayo soko kubwa la mazao yake lipo Mashariki ya kati . Kwa hali hiyo bei za vyakula kwa nchi za Mashariki ya kati zinatarajiwa kupanda na kupelekea wakaazi wake ambao wengi wao ni wageni toka nchi za nje kuzama zaidi mfukoni .

Hatua muhimu ambazo serikali inatakiwa kuzichukua kabla "hatujaelekea kula kwa kushiba moshi" ni kubana matumizi yake hasa posho za vikao na misafara ya wakubwa.Mfano mzuri ni matukio ya hivi karibuni kwa Waziri Mkuu(Mtoto wa mkulima)  kukataa gari la kifahari na kitendo cha waziri wa fedha Mustafa Mkullo kufanya ubadhirifu kwa kukodi ndege na kuagiza kupelekewa gari lake Dodoma .

Kilimo kwanza lazima kutiliwa mkazo wa hali ya juu kwani ongezeko la bei ya chakula linahatarisha amani ya wananchi.Mara nyingi tunapoona ndiyo tunapopata fundisho, siku za hivi karibuni nchi ya  Tunisia imejikuta ikikabiliwa na maandamano kutokana na halingumu ya maisha iliyotokana na ongezeko la watu  kukosa ajira.
Nathubutu kusema hivyo kutokana na kuwa "njaa ikiingia mlangoni ,amani hutokea dirishani" uvumilivu una kiasi chake nacho nikupatiwa ufumbuzi ili nafuu ya maisha ipatikane.

Serikali inatakiwa kujipanga vizuri ilikujikwamua kiuchumi bila kutarajia huruma za wahisani kufanikisha bajeti zetu, ni kwa kutumia vyema raslimali zetu kama bandari,viwanja vya ndege, vivutio vya utalii ,ardhi yenye rutuba,madini na gesi.

Hayo yote yakiwezekana Tanzania haitakuwa tena ikitembeza kikapu kwa wahisani zetu, kwani dunia ya sasa "Tunaelekea kula kwa kushiba Moshi" .



No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...