Wakuu wa Serikali Ya Umoja wa Kitaifa wa Kenya wapuuzia taarifa ya WIILEAKS
Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga Akizungumza jambo,huku pembeni yake
Rais Mwai Kibaki akimsikiza.
Serikali ya Kenya imepuuzilia mbali taarifa zilizofichuliwa na tovuti ya Wikileaks ambazo zinamnukuu balozi wa Marekani nchini humo, Micheal Rannenberger, akisema kwamba Rais Mwai Kibaki na waziri mkuu Raila Odinga ndio kikwazo kikuu katika kuleta mageuzi nchini Kenya.
Balozi huyo pia alinukuliwa akisema serikali ya Marekani haitasita kuendesha kampeni kupitia makundi ya kiraia ili kuhakikisha mabadiliko yanafanyika.
Akizungumza na BBC akiwa jijini London, Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga amemshutumu bwana Rannenberger kwa kuwa mnafiki. ''Taarifa zinazotolewa na WikiLeaks ni uvumi mtupu. Yale yote yaliyomo ni masengenyo. Ni watu wanaokusengenya, wanayozungumza kukuhusu hadharani ni tofauti na yale wanayozungumza kisiri,'' akasema bwana Raila.
Kuhusu madai kuwa yeye na rais Kibaki hawakuchukuwa hatua zozote kwa kutekeleza mageuzi yanayohitajika, ili kuhakikisha kuwa machafuko ya baada ya uchaguzi kama yale yaliyoshuhudiwa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 yatokee tena bw Raila amesema, '' Bwana Ranneberger anaishi nchini Kenya kama mgeni. Iwapo anataka kutushauri ana haki ya kufanya hivyo. Lakini vile vile wageni ni sharti watuheshimu''.
Nayo taarifa kutoka ikulu ya rais ya Nairobi imepuuzilia mbali madai hayo ya balozi wa Marekani kwa kusisitiza kuwa rais Mwai Kibaki ana historia nzuri ya kutekeleza mageuzi kwa kufanikisha kuidhinisha kwa katiba mpya ya taifa hilo.
Taarifa hizo za kisiri, ni miongoni mwa stakabadhi ambazo zimefichuliwa na tovuti ya Wikileaks , kuhusiana na nchi ya Kenya na viongozi wake.
Chanzo: BBC
No comments:
Post a Comment