Rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki yumo mjini Abidjan kuongoza juhudi za upatanishi, huku jeshi la Côte d'Ivoire, likiifungua mipaka ya anga, majini na ardhini ya taifa hilo
Kiongozi wa upinzani nchini Côte d'Ivoire, Alassane Ouattara, ambaye anadai ndiye rais mpya wa nchi hiyo, amesema rais wa sasa Laurent Gbagbo lazima ajiuzulu baada ya uchaguzi uliozusha mzozo nchini humo. Ouattara ameyasema hayo baada ya kukutana na rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, anayeongoza juhudi za upatanishi nchini Côte d'Ivoire. Ouattara amemwambia Mbeki kwamba yeye ndiye rais halali wa Côte d'Ivoire na kumtaka amshawishi rais Gbagbo aondoke madarakani baada ya kushindwa katika uchaguzi. Bwana Mbeki aliyewasili jana mjini Abidjan amesema wanataka kusikiliza maoni yote kuhusu suala hilo kabla kutoa mapendekezo yoyote.Ouattara ametangaza serikali yake na kumteua waziri mkuu wa zamani wa serikali ya Gbagbo, Guillaume Soro, kama waziri mkuu mpya atakayekuwa pia waziri wa ulinzi. Rais Gbagbo aliapishwa Jumamosi iliyopita ingawa tume ya uchaguzi ya Côte d'Ivoire ilimtangaza Ouattara kama mshindi wa uchaguzi wa Novemba 28 mwaka huu, matokeo ambayo yalithibitishwa na Umoja wa Mataifa. Wakati huo huo, jeshi la Côte d'Ivoire limetangaza kuwa mipaka yote ya nchi hiyo imefunguliwa kuanzia saa kumi na mbili asubuhi ya leo. Haikubainika wazi kwa nini jeshi hilo limeamua kuifungua mipaka wakati huu.
Chanzo:Dw Swahili
No comments:
Post a Comment