KUNDI la wahisani wanaochangia bajeti kuu ya Tanzania (GBS) limeibua kashfa baada ya kueleza kuwa serikali iliwapelekea bajeti tofauti na ile iliyopitishwa na Bunge Julai mwaka huu.Taarifa za kashfa hiyo ziliwekwa hadharani jana asubuhi na mwenyekiti wa wahisani hao, Svein Baera wa Sweden katika mkutano wa kitaifa wa mwaka wa majadiliano ya kisera na bajeti uliofanyika jijini Dar es salaam.
Sweden ndiyo inayoshikilia uenyekiti wa kundi hilo linalojumuisha taasisi za kimataifa na nchi mbalimbali zilizoendelea.
Kuibuliwa kwa kashfa hiyo kunakuja wakati wahisani hao wakiwa wamezuia theluthi moja ya zaidi ya dola 800 milioni za Kimarekani ambazo zinatakiwa zichangie kwenye bajeti kuu ya 2010/11, wakiishinikiza serikali iharakishe utekelezaji wa programu ya mageuzi, yakiwemo ya mfumo wa usimamizi wa fedha za seikali.
Akitoa hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo wa siku tatu, Baera aliainisha maeneo sita kuwa ndiyo mhimili wa mjadala wao na serikali.
"Napenda kuainisha maeneo sita ya ujumbe wetu ili kuweka sawa jukwaa la majadiliano yetu haya ya mwaka. Kuna tofauti kati ya bajeti iliyowasilishwa kwa bodi ya (Shirika la Kimataifa la Fedha) IMF na ile iliyopitishwa na Bunge Julai 2010," alisema Baera.
Alisema bajeti ambayo serikali iliwasilisha kwa wahisani hao ilibeba "matumaini makubwa ya kuzaa matokeo mazuri na kufanywa kama sababu ya kupitisha matumizi makubwa ya fedha zitokanazo na mapato ya ndani".
Baera alisema kuwa kukosekana kwa uwazi katika matumizi, vipaumbele, mapato na mfumo mzima wa fedha kunapunguza kuaminika kwa bajeti hiyo mbele ya wafadhili.
Kwa mujibu wa wahisani hao, kumekuwepo na mtiririko wa athari katika bajeti katika miaka ya karibuni huku ikionyesha ongezeko kubwa la matumizi ya kawaida kuliko yale ya maendeleo.
Kwa mujibu wa bajeti ya mwaka 2010/11 ambayo ni ya Sh11.1 trilioni, matumizi ya kawaida ya serikali ni Sh7.8 trilioni wakati fedha zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo ni Sh3.2 trilioni.
Bajeti hiyo inaonyesha kuwa kati ya Sh11.1 trilioni, serikali ilitarajia kupata Sh6 trilioni kutoka katika vyanzo vya ndani, wakati inatarajia Sh2.8 trilioni kutoka kwa wahisani na mikopo. Fedha nyingine zinatarajiwa kutoka mikopo ya ndani, masharti ya kibiashara na ubinafsishaji.
"Matumaini makubwa kupindukia katika bajeti hii na kutokuwepo kwa mikakati inayoeleweka ya kipaumbele katika matumizi katika hali inayoweza kutokea ya mapato madogo na ukosefu wa fedha, yanaweza kuondoa kuaminika kwa bajeti kama chombo cha ufanisi wa sera na mipango," alisema Baera.
Zaidi ya hapo, ukweli kwamba bajeti hii tofauti ilipitishwa bila ya kuwepo mawasiliano ya awali na wabia wa maendeleo inaweka maswali kwenye ubora wa mazungumzo yetu ya sera na ubia. Tunatarajia kujadili suala hili kwenye sehemu muhimu ya bajeti.
"Zaidi ya hapo, bajeti iliyotumiwa kuanzia mwaka jana iliendeleza mwenendo wa miaka ya karibuni ambako matumizi ya kawaida yanaendelea kupanda kwa kasi kuliko matumizi kwenye maendeleo."
Kutokana na hali hiyo GBS imeitaka serikali kujipanga upya na kuweka mkazo katika kupunguza misamaha ya kodi ili kuweka uwiano na ufanisi sawa na nchi za kundi lake katika uchumi, hatua ambayo Baera alisema itapunguza pengo la bajeti linaloikabili Tanzania kila mwaka.
Tayari GBS imebainisha kuwa bajeti ijayo inaweza kuwa na nakisi ya hadi Sh1 bilioni.
Hata hivyo, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo ambaye alishiriki mkutano huo, alipatwa na kigugumizi kujibu madai hayo ya GBS, akimkaribisha mwenyekiti huyo wa kundi la nchi wahisani aende ofisini kwake ili wazungumzie masuala hayo.
"Kuna mengine yanazungumzika; Baera ninakukaribisha ofisini kwangu; mengine yanazungumzika ofisini," alisema Mkulo.
Naibu kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Zitto Kabwe alizungumzia kasoro hiyo jana akieleza kuwa imemshtua na kwamba ataifuatilia.
Zitto, ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Kaskazini na ambaye alihudhuria mkutano huo jana, alisema kambi ya upinzani itaunda kamati kulifuatilia suala hilo.
Alisema pia watahoji suala hilo bungeni na kuitaka serikali iweke wazi kwa Watanzania ni bajeti ipi inayotumika kati ya iliyopitishwa na Bunge na ile iliyopelekwa IMF.
"Huu ni mshtuko kwangu; hili limenishtua. Tutaunda timu ya kulifuatilia; tutalifikisha bungeni na kuihoji serikali ieleze ni bajeti ipi inayotumika. Ni ile iliyopitishwa na Bunge au iliyopelekwa IMF," alisema Zitto.
Kundi hilo la nchi wahisni limesema kuwa linaunga mkono mkakati wa serikali wa Kilimo Kwanza na wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) kuhusu maendeleo ya kilimo, hifadhi ya chakula na kupunguza umasikini.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment