Mtazamohalisi

Saturday, December 11, 2010

Bakari Abeid Gwiji La Sanaa Z'bar Afariki Dunia

Marehemu Bakari Abeid
  Marehemu Bakari Abeid(1933-2010)

Na Salum Vuai
KAMBI ya wasanii wa fani za taarab na maigizo nchini, imegubikwa na msiba kwa kuondokewa na msanii gwiji na mkongwe Bakari Abeid Ali aliyefariki jana alfajiri nyumbani kwake Mombasa mbuyu mnene.

Marehemu huyo (77) amekutwa na mauti baada ya kukumbwa na maradhi ya kiharusi yaliyomsumbua kwa muda mrefu.

Msanii huyo aliyezaliwa Agosti 25, 1933 katika kijiji cha Ole kisiwani Pemba, atakumbukwa kwa umahiri wake katika sanaa za utunzi, uimbaji taarab na maigizo, ambapo aliweza kuwavutia mashabiki wengi katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Wakati wa uhai wake katika enzi alizojikita kikamilifu katika usanii, Abeid alikuwa hodari wa kuwatuliza watazamaji alipokuwa jukwaani kwa namna alivyomudu kuiteka hadhira kwa umahiri wake wa kuigiza na kuimba.

Baada ya kudhihirisha kipaji chake, marehemu aliwahi kuwa mwanachama wa vyama tafauti vya taarab ikiwemo Michenzani alichoshiriki kukiasisi mwaka 1952, Nadi Ikhwan Safaa (1956) na Culture (1964).

Akiwa msanii mashuhuri, marehemu alishiriki kutunga na kuimba au kutia muziki nyimbo mbalimbali katika vikundi hivyo na miongoni mwa hizo ni ‘Mazowea yana tabu’, ‘Njiwa peleka salamu’, ‘Tini tunda la tamasha’, ‘Pendo halijui siri’, ‘Bahati’, ‘Kisebusebu’, ‘Wagombanao hupatana’, ‘Nnapenda kwa ishara’ na nyengine nyingi.

Mbali na shughuli za kisanii, marehemu Bakari Abeid alifanya kazi serikalini na kushika nyadhifa kadhaa kwa vipindi tafauti kama vile Afisa wa Sanaa katika Wizara ya Habari, Utamaduni na Utalii (1985), Mjumbe wa Baraza la Sanaa Tanzania (1986), Mjumbe Baraza la Sanaa Zanzibar (BASAZA) mwaka 1989.

Aidha aliwahi kuwa Mkuu wa Habari, na baadae wa utangazaji katika Idara ya Habari na Utangazaji Zanzibar, Mkuu wa Vipindi Televisheni Zanzibar na Mshauri wa Rais mambo ya utamaduni na pia mshereheshaji mkuu katika sherehe mbalimbali za kitaifa.

Wananchi wengi watamkumbuka kwa kipindi kilichompatia umaarufu mkubwa katikaSauti ya Tanzania Zanzibar cha ‘Ndivyo tulivyo, akishirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Abdallah Mwinyi Khamis ambacho baadae kilihamia Televisheni Zanzibar.

Marehemu aliyezikwa jana katika makaburi ya Mwanakwerekwe ambapo mazishi yake yalihudhuriwa na mamia ya wananchi wakiwemo wasanii wa fani mbalimbali, ameacha mtoto mmoja wa kiume.

Gazeti la SMZ.na Mzalendo

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...