BAADHI ya wafanyakazi wa ubalozi wa China , jijini Dar es Salaam, wanadaiwa kushirikiana na wezi wa kuvunja magari ya watu wanaofika ubalozini hapo.
Kumekuwa na matukio ya uhalifu katika ubalozi huo na Tanzania Daima ilifika katika eneo na kukuta vijana wakizagaa hovyo nje ya jengo la ubalozi hasa katika eneo la maegesho ya magari ambako uhalifu huo unafanyika.
Kadhalika ulinzi katika ubalozi huo uko ndani tu hali ambayo husababisha usumbufu na hasara kwa watu ambao wanakwenda katika ubalozi huo kwa shughuli za kikazi na kuegesha magari yao nje.
Wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya watu ambao wamekumbwa na mkasa wa kuibiwa katika eneo hilo la maegesho ya magari ubalozini hapo walisema watu wanaofanya uhalifu huo ni wa rika tofauti tofauti na wamekuwa wakivinjari katika ubalozi huo bila shughuli yoyote muhimu.
Katika tukio la hivi karibuni, gari la Mkurugenzi Mtendaji na mmiliki wa maduka ya vipodozi ya Shear Illusions Shekha Nasser, lilivunjwa na kuibiwa Laptop moja, fedha taslimu kiasi cha sh 250,000, tiketi ya ndege moja na vitabu vya hundi viwili vya benki ya CRDB na NMB, funguo za maduka na vitu vingine mbalimbali.
Shekha alisema tayari amefungua jalada lenye RB OB/RB/21477/2010 katika kituo cha Polisi Oysterbay, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Shekha, mara baada ya kuibiwa alimueleza mlinzi aliyekuwepo katika ubalozi huo, lakini jambo la kushangaza alimjibu kuwa hashangazwi na tukio hilo kwani vitendo hivyo vimeota mizizi na kukiri kwamba kwa siku huwa watu watano hadi sita huibiwa na kazi ya kulinda magari siyo ya kwao bali ni ya Jeshi la Polisi.
Tanzania Daima ilifanikiwa kufika eneo la ubalozi huo uliopo katika maeneo ya Oysterbay na kushuhudia hali ya hatari nje ya ubalozi kutokana na kukosekana ulinzi kama zilivyo balozi nyingine.
Kadhalika watu wanaoranda randa katika ubalozi huo wanadai kuwa wao ni mawakala wa kusaidia watu kupata pasi za kusafiria.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment