Mtazamohalisi
Thursday, December 30, 2010
Waziri Akataa Kuuziwa Mkaa Korogwe
Waziri wa Maliasili na Utalii,Ezekiel Maige
Wauza mkaa katika eneo la kijiji cha Chekeleni, wilayani Korogwe mkoani Tanga, walivamia gari la Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, baada ya kusimama ghafla katika eneo hilo na kutaka wamuuzie mkaa wao, wakifikiri ni mteja wa kawaida.
Hata hivyo, ndoto za wafanyabiashara hao ziliyeyuka ghafla, baada ya kubaini kwamba, Waziri Maige si mteja kama walivyofikiria, bali alisimama hapo kutaka kuona kama wanauza mkaa huo kihalali.
Baada ya kugundua kwamba wanayemshawishi anunue mkaa wao ndiye Waziri wa Maliasili na Utalii, wafanyabiashara hao waliokuwa wamepanga maguni ya mkaa pembezoni mwa barabara, waliamua kutimua mbio na kuacha mkaa wao, huku waliobaki katika eneo hilo, wakikana kujihusisha na biashara hiyo.
Waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wa Waziri Maige, walipata fursa ya kuzungumza na baadhi ya wananchi ambapo walidai kuwa wamekuwa wakiuza mkaa kwa Shilingi 7,500 kwa gunia moja.
Wananchi hao walisema kuwa wamekuwa wakiuza mkaa huo kila siku ili waweze kujipatia ridhiki na kwamba baadhi ya maafisa misitu wamekuwa wakiwaomba chochote (rushwa) ili wawaruhusu kuendesha biashara hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa ushuru wa Sh. 1,000.
“Hata hivyo, tunashindwa kuelewa maana mara waje watu wengine na kujiita watu wa TRA, tunawapa ushuru na tunaposhindwa kutoa wanachukua mkaa na kuondoka nao. Mara nyingine wanakuja watu wa halmashauri tunatoa ushuru gunia Sh. 1,000,” alisema mwananchi mmoja na kuoinyesha risiti ya magunia 50.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Athuman Said, alirusha lawama kwa baadhi ya watumishi wa serikali kwamba wao ndio chanzo cha ushuru wa mazao ya misitu kupotea kwa sababu wamekuwa hawatekelezi majukumu yao ipasavyo.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo ameishauri serikali kuwabana wachoma mkaa ili waweze kutoa ushuru badala ya kuwabana wafanyabiashara wadogo wadogo tu.
Kwa upande wake, Waziri Maige, aliagiza kwamba maafisa misitu wahakikishe kila anayefanya biashara ya mkaa anatoa ushuru wa Shilingi. 2,000 kwa gunia moja na kwamba wasimamie ipasavyo sheria namba 14 ya mwaka 2004, inayohusu mazao ya misitu.
Waziri Maige aliwataka wananchi kuhakikisha pindi wanaponunua mkaa wapewe risti, ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza na kwamba wakikutwa wakiwa hawana risti watakamatwa kwa mjibu wa sheria.
Waziri Maige aliwaambia wananchi hao kuwa kudai risiti kutasaidia kukusanya mapato ya serikali kwa kiwango kinachotakiwa kwani wakwepaji wa ushuru watakuwa wamedhibitiwa.
“Wananchi wahakikishe pindi wanapouziwa mkaa wapewe risti na muuzaji huyo, maana ukikamtwa huna risiti ni kosa. Na hali hiyo itasaidi kuwabana wakwepaji wa ushuru na hivyo kukusanya mapato ya serikali vizuri,” alisema Waziri Maige, ambaye tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo mwezi uliopita, amekuwa akichukua hatua za kubana wizi wa rasilimali za nchi.
Chanzo: Nipashe
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment