Mtazamohalisi

Monday, December 27, 2010

Sitta Asubiria Taarifa Rasmi Kuhusu Hoja Ya Mgeja

Vinara wakukemea ufisadi

Waziri wa ushirikiano wa Afrika Mashariki,Spika wa
mstaafu Samuel Sitta akiwa na Mbunge wa SameMashariki
Bi Anna Kilango.

WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amesema amasubiri kwa hamu hoja binafsi iliyoahidiwa kuwasilishwa Halmashauri Kuu ya CCM na Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja,.

Alhamisi iliyopita, Mgeja alimtuhumu Sitta kuwa anaendeleza mgawanyiko ndani ya CCM na kumtaka afute kauli yake kuwa aliondolewa uspika kwa mizengwe, la sivyo atawasilisha hoja binafsi Nec kumtaka athibitishe. 
“Sitta anapaswa kufuta kauli yake kuwa, aliondolewa kwa hila…kikao kilichofanya uamuzi kuhusu nafasi ya uspika ni Kamati Kuu ya CCM. Kwa hiyo anamaanisha wajumbe wa kikao hicho wana hila naye.

Kusema hivyo kutasababisha baadhi ya wanachama kukosa imani na kikao hicho,” alisema Mgeja. 
Akizungumza na gazeti hili juzi, Sitta alisema ingawa hajapata taarifa rasmi kuhusu hoja za Mgeja, anaisubiri kwa hamu.

“Siwezi kuzungumzia kwa kina taarifa ya Mgeja kwa kuwa sijaipata vizuri, lakini ninaisubiri kwa hamu hoja yake hiyo,’’ alisema Sitta ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Tisa.

Wakati Sitta akisita kujibu hoja ya Mgeja, Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango, amemshangaa Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa wa Shinyanga, akisema alichosema hakiwezekani.
Pia, Kilango alipuuza msimamo wa Mgeja akisema hauna mashiko: "Hoja binafsi zinapelekwa bungeni tu, sio kwenye vikao vya chama. Vikaoni zinaletwa ajenda, sasa huoni haya ni maajabu?"

“Huyu mwenyekiti asituvuruge, tunatakiwa kujua chama kinaelekea wapi na tumefikaje hapa,” alisema Kilango na kueleza kuwa anaamini Mgeja katumwa, huku akiongeza:

"Ni bora pia atwambie (Mgeja) ametumwa na nani kwa kuwa anachozungumza ni kudanganya umma."

Kilango ambaye alikuwa akizungumza kwenye mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwake jijini Dar es Salaam jana, alisema anamshangaa mwenyekiti huyo kumwandama Sitta, badala ya kutafakari jinsi alivyopoteza majimbo manne ya ubunge mkoani Shinyanga.

"Huyu anataka tumkate panya mkia halafu aendelee kuishi badala ya kumkata kichwa ili kumaliza tatizo," alisema Kilango akimaanisha kuwa Mgeja anataka kukwepa hoja ya msingi kwa kuanza kuzungumzia mambo yasiyomhusu.

"Namsihi Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, asikubali kuwa na viongozi ndani ya chama ambao wanataka kumkata panya mkia badala ya kumkata shingo ili afe," alisema Kilango.

Alisema hivi sasa CCM inatakiwa kuokoa chama kwa kufanya tathmini kujua chanzo cha wananchi kuwakataa, lakini sio kuzungumzia mambo yasiyo na msingi.

Desemba 19, mwaka huu, Sitta alitoa kauli nyingine inayoweza kutikisa CCM baada ya kueleza kuwa, aliondolewa kwenye kinyang'anyiro cha Spika wa Bunge kutokana na hila za viongozi, ambao walishindwa kuhimili kasi ya utendaji wake kwenye chombo cha kutunga sheria.

Mbunge huyo wa Urambo Mashariki, alijikuta akianguka kwenye kinyang'anyiro hicho baada ya CCM kwa kile kilichoelezwa kuwapa wanawake nafasi ya kuongoza moja ya mihimili ya nchi.
Chanzo: Mwananchi.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...