Mtazamohalisi

Wednesday, December 29, 2010

Dk. Slaa Aacha Kilio CCM

USHINDI mwembamba wa Chama cha Mapinduzi (CCM) uliosababisha ruzuku yake kuporomoka, umekiweka chama hicho mahali pabaya baada ya watendaji wake kushindwa kulipana mishahara.

Chama hicho tawala kimefikia hatua ya kushindwa kuwalipa watendaji wake hasa wale wa nchini na kupunguza matumizi baada ya ruzuku yake kushuka kutoka zaidi ya sh bilioni moja hadi sh milioni 800,000 baada ya mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willbrod Slaa kupunguza kura za Rais Jakaya Kikwete kwa kiwango kikubwa.

Habari kutoka ndani ya makao makuu ya CCM, zinasema chama hicho kimepunguza matumizi yake kwa kiasi kikubwa na mara nyingi Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusuf Makamba, amekuwa akiwaambia watendaji hao kwamba hali hiyo inatokana na kupungua kwa ruzuku.

'Sasa hivi hakuna cha vocha wala pesa za posho kama zamani. Tunaambiwa tujitolee, watendaji wa chini waliokuwa wakipelekewa pesa kila mwezi, kama hawawezi kujiendesha, wasitegemee pesa toka makao makuu,' alisema mmoja wa maafisa wa chama hicho, ofisi ndogo ya Lumumba, Dar es Salaam.

Mbali ya kushindwa kulipana mishahara, habari zaidi zinasema watu walioathirika na kimbunga cha Dk. Slaa ni taasisi za CCM ambazo ndizo zilikuwa kinara wa kumpinga Dk. Slaa wakati wa kampeni.

Taasisi hizo zinazomegewa ruzuku kila mwezi mgao wao umepungua na kuna uwezekano wa baadhi yao kufutiwa kabisa.

Baadhi ya taasisi zinazopata ruzuku toka makao makuu ya CCM ni pamoja na kundi la muziki wa dansi, kwaya na maigizo la Tanzania One Theatre (TOT), Radio Uhuru, Kampuni ya Magazeti ya Uhuru na Mzalendo, jumuiya za chama ambazo ni Umoja wa Vijana (UVCCM), Jumuiya ya Wanawake (UWT) na Jumuiya ya Wazee CCM (TAPA).

'Kwanza TOT, magazeti ya Uhuru na Mzalendo na Radio Uhuru, yanaweza kufutiwa kabisa ruzuku maana hakuna maana ya kuwapa ruzuku kama wanapaswa kujiendesha kibiashara na wanapata faida. Mpango huo umeanza kujadiliwa sana pale makao makuu,' alisema mmoja wa makada wa CCM ambaye ni mjumbe wa Halmashauri Kuu.

CCM inapata kiwango sh milioni 800 kutokana na kupata asilimia 60.40 ya kura za urais katika uchaguzi huo, ambazo ni sawa na sh milioni 354 na asilimia 77 ya wabunge (sawa na sh milioni 460) kwa mwezi.

CHADEMA inapata sh milioni 203.6, kwa kupata asilimia 24 ya kura za urais (sawa na sh milioni 146) na asilimia 9.62 ya wabunge (sawa na sh milioni 56) wakati CUF, sasa inapata sh milioni 117.4, kutokana na kupata asilimia 9.80 ya kura za urais (sawa na sh milioni 57.9) na asilimia 10 ya wabunge (sawa na sh milioni 56).

NCCR-Mageuzi inapata ruzuku ya sh milioni 10 kutokana na kupata asilimia 1.08 ya wabunge wakati UDP na TLP vinapata ruzuku ya sh milioni 2.4 kwa kupata asilimia 0.42 ya kura za ubunge kila kimoja.

Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi, ruzuku hiyo hutolewa kwa chama kilichofikisha kuanzia asilimia tano ya kura za urais na kwa uwiano wa wabunge na madiwani, ambao chama kilivuna katika uchaguzi huo.

Ruzuku hiyo ilianza kutolewa Novemba, baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika nchini Oktoba 31, mwaka huu na ule uliofanyika baadaye katika baadhi ya majimbo kukamilisha uchaguzi huo.

Katika uchaguzi mkuu uliopita, Rais Kikwete alipata ushindi mwembamba wa kura milioni tano, sawa na asilimia 61.17, akifuatiwa na Dk. Slaa aliyepata kura 2,271,941, sawa na asilimia 26.34, wakati mgombea wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba aliambulia kura 695,667, sawa na asilimia 8.

Chanzo: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...