Mtazamohalisi

Monday, December 20, 2010

Sitta: Nilitemwa uspika kwa hila za vigogo

Wastaafu wakibadilishana mawazo ya uongozi

Toka shoto Waziri mkuu mstaafu Edward Lowasa
na kulia ni Spika Mstaafu Samuel Sitta.

WAZIRI wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta jana alitoa kauli nyingine inayoweza kukitikisa chama chake cha CCM baada ya kueleza kuwa aliondolewa kwenye kinyang'anyiro cha kiti cha spika wa Bunge la Muungano kutokana na hila za viongozi ambao walishindwa kuhimili kasi ya utendaji wake kwenye chombo hicho cha kutunga sheria.


Sitta, ambaye alipata umaarufu baada ya kuliongoza Bunge la Tisa kwa mafanikio, ametoa kauli hiyo wiki chache baada ya kukaririwa na vyombo vya habari akisema bayana kuwa kuilipa kampuni tata ya Dowans fidia iliyoamuliwa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kibiashara (ICC) ni sawa na kuhujumu uchumi.

Mbunge huyo wa Urambo Mashariki alijikuta akianguka kwenye kinyang'anyiro cha uspika wa Bunge la Kumi baada ya chama chake cha CCM kuamua kuwapa wanawake nafasi ya kuongoza moja ya mihimili ya nchi na hivyo kupitisha wagombea watatu wanawake katika mchakato uliompa ushindi Anne Makinda.

Jana, Sitta ambaye alikuwa akihojiwa na Mwananchi, alisema utendaji wake wa kasi na viwango uliwatisha viongozi wengi wa serikali na ndio maana wakaamua kutumia kigezo cha jinsia kumwondoa.
"Unajua nataka hili ilieleweke; juzi nilienda jimboni kwangu Urambo Mashariki nikawaeleza wapiga kura wangu kwa nini sasa mimi sio spika tena, maana wanaweza kudanganywa kama kazi imenishinda au nimefukuzwa," alisema Sitta.

"Watanzania lazima wajue mimi sijafukuzwa kazi wala sijashindwa kufanya kazi hiyo, ila kuna viongozi ambao ni wakuu wangu ndani ya chama chetu ambao wameshindwa kuendana na kasi na viwango vyangu ndio maana wakaamua kuweka sharti ambalo kamwe nisingeweza kulitimiza.

"Kigezo hicho cha jinsia walikileta katika hatua za mwisho za mchakato wa kumtafuta spika wakijua kwamba sitaweza kukitimiza na ningejua hilo mapema, nisingepeleka jina langu kuomba kuteuliwa tena."

Sitta alisema ni wazi kamba asingeweza kutimiza sharti kwamba spika aliyetakiwa safari hii ni mwanamke ndio maana hakuweza kuteuliwa tena kuwania nafsi hiyo.

"Mimi ni Sitta na nitabaki kuwa Sitita yule yule kama nilivyozaliwa na kwa vyovyote vile; nisingeweza kufanya chochote ili kuhakikisha sharti hilo nalitimiza," alisema Sitta.

Hata hivyo Sitta alisema kuwa endapo jina lake lingepitishwa, alikuwa na ukakika wa kurudi katika kiti hicho kwa kuwa asilimia kubwa ya wabunge walikuwa wameukubali utendaji wake.

Katika miaka ya mwisho ya uongozi wake wa Bunge la Tisa, Sitta alikuwa akilalamikia kuwepo kwa njama alizodai zinafanywa na mafisadi kutaka kumuangusha kwenye ubunge na wakati fulani alifikia hadi kuomba ulinzi zaidi kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda akisema anatishiwa maisha.

Sitta hajawahi kuwataka hadharani wapinazani wake, lakini baadhi ya vyombo vya habari viliwahi kumuhusisha na vita vya uwaziri mkuu, lakini akakanusha vikali akisema kama angetaka nafasi hiyo asingegombea uspika.

Sitta aliwataka wapigakura wake na Watanzania kwa ujumla kutosikitishwa na kitendo cha kuenguliwa kwenye kinyang'anyiro cha uspika, akisema kuwa anaamini bado Rais Jakaya Kikwete anawapenda watu wa Urambo na kuendelea kuwaheshimu ndio maana amemteua kushika dhamana nyingine.

"Nawaahidi Watanzania huu sio mwisho wa utendaji wangu wa kazi sasa kasi na viwango navihamishia katika Wizara hii muhimu na kwamba wananchi wasiogope tena Tanzania kuingia katika Shirikisho la Afrika Mashariki,"alisema.

Alisema akiwa Waziri wa Afrika Mashariki atahakikisha Watanzania wanafaidika na shirikisho hilo na kwamba suala la ardhi halitakuwepo kwa kuwa tahadhari zote zimechukuliwa.

Sitta alifanya ziara kwenye jimbo lake la Urambo Mashariki ambako pamoja na mambo mengine, alihudhuria mkutano wa uchaguzi wa mwenyekiti wa halmshauri ya Urambo.

Katika mkutano huo, Alhaji Adam Malunkwi wa CCM alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa halmashauri hiyo.
Kabla ya mkutano huo, Sitta, ambaye alipokewa na wapigakura wake kwa msafara wa pikipiki zaidi ya 70, magari zaidi ya 40 na vikundi mbalimbali vya hamasa, alitumia fursa hiyo kuwaeleza wapigakura hao kilichomfanya ashindwe kutetea nafasi yake ya uspika.

Sitta pia alitoa msaada wa mashine ya kusaga na kukoboa nafaka kwa kikundi cha kinamama wa Uyogo kutekeleza ahadi yake kabla ya uchaguzi mkuu

Alisema mashine hiyo itakuwa kitega uchumi chao kwa kile anachoamini kuwa ukimwezesha mama, umeiwezesha jamii.

Mbali na mashine hiyo Sitta pia alitoa msaada wa mashine ya umeme wa sola kwa ajili ya zahanati ya Uyogo.

Akikabidhi msaada huo alisema kabla ya umeme haujasambaa maeneo hayo, atahakikisha zahanati zote zinapata umeme huo kurahisisha huduma zake kwa jamii.

Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...