Serikali imeiagiza Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), kuvunja mkataba na Kampuni ya Udalali ya Majembe Auction Mart ya jijini Dar es Salaam Desemba 31, mwaka huu.
Majembe ilipewa na Sumatra mkataba wa uwakala wa kusimamia shughuli za daladala jijini Dar es Salaam kwa miaka miwili kuanzia mapema mwaka huu.
Akizungumza na Waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu, alisema kuvunjwa kwa mkataba huo kutasaidia kupunguza kero zinazosababishwa na Majembe.
Nundu alisema wameamua kuuvunja mkataba huo kutokana na Majembe kuendelea kukiuka sheria na kanuni walizopewa wakati wa kabla ya kuanza kufanya kazi za uwakala.
Kwa Mujibu wa Waziri huyo, Majembe ilianza kufanya kazi ambazo haziwahusu na ambazo hawana ujuzi nazo, ikiwa ni pamoja na zile za usalama barabarani.
Alisema zipo baadhi ya kazi zinazotakiwa kufanya na askari wa kikosi cha usalama barabarani, lakini kinyume chake zimekuwa zikifanywa na Majembe, jambo ambalo ni kuingilia kazi zisizowahusu.
" Hii siyo sawa, hatutakiwi kuweka watu watufanyie kazi wasizo na uzoefu nazo…lazima tuweke mfumo madhubuti utakaotusaidia kutatua matatizo, si kuweka weka tu, watu wasio na utaalamu," alisisitiza.
Alisema baadhi ya kazi ambazo ni kinyume na sheria zinazofanywa na Majembe ni pamoja na kukagua magurudumu ya magari, leseni, bima, taa za magari na vioo.
Waziri huyo alisema ikiwa Sumatra watahitaji kuendelea kufanya kazi na Majembe, wanatakiwa wawape mafunzo maofisa wake kwanza kuhusu namna kufuata sheria za usalama barabarani.
Sumatra iliipa Kampuni hiyo mkataba huo kwa lengo la kuboresha usafiri wa umma na kuondoa kero kwa wakazi wa Dar es Salaam, kusimamia, kufuatia na kufanya ukaguzi wa utekelezaji wa masharti ya leseni.
Kabla Majembe haijapewa mkataba huo, wakazi wa Dar es Salaam walikuwa wakilalamikia vitendo vya ukiukwaji wa sheria vilivyokuwa vikifanywa na daladala kama kukatisha safari, kushusha na kupakia abiria katika maeneo yasiyo na vituo, makondakta na madereva kutovaa sare, kutoza nauli za juu, matusi na kukataa kuwabeba wanafunzi.
Moja ya sababu ambazo hivi karibuni zilikuwa zikilalamikiwa na wamiliki wa mabasi ya mikoani na daladala dhidi ya Sumatra ni kuiruhusu Majembe kuweka wafanyakazi kufanya kazi za barabarani.
Mapema mwezi huu, wamiliki wa mabasi walitishia kugoma pamoja na mambo mengine, wakitaka kampuni hiyo isijihusishe na kazi za barabarani bila kuwepo na askari wa kikosi cha usalama barabarani..
Wakati huo huo; Serikali imetangaza kuwaondoa mara moja wapiga debe katika vituo vyote vya mabasi nchini.
Nundu alizitaka mamlaka zinazohusika kuandaa utaratibu wa kuwatambua wafanyakazi na mawakala wa makampuni ya mabasi kwa kuwapatia vitambulisho maalum.
Alisema utaratibu wa kuhakikisha wapiga debe wanaondoka katika vituo vya mabasi unatakiwa kufanyika sasa na kwamba ifikapo Januari 15, mwakani, utaratibu wa kutoa vitamburisho kwa wafanyakazi na mawakala unatakiwa uwe umekamilika.
" Ninaagiza kwamba kuanzia sasa ninataka kuona wapiga debe wote wameondolewa katika vituo vyote vya mabasi, na zoezi hili linatakiwa kufanyika haraka iwezekanavyo,” alisema.
Aliongeza kuwa wapigadebe wamekuwa kero kubwa kwa wasafiri hususani wa mikoani kusumbuliwa wanapokwenda kukata tiketi na wakati mwingine kuwaibia.
Kwa upande mwingine, Nundu alisema kuna umuhimu wa kuwepo kwa matuta barabarani ili kupunguza ajali zinazotokana na mwendo kasi.
Alisema Wizara yake kwa kushirikiana na ya Ujenzi, itachukua hatua mwafaka ili kuhakikisha ujenzi wa matuta barabarani unafuata viwango.
Alisema ukosefu wa matuta barabarani pia umekuwa ukisababisha uharibifu wa mabasi na hivyo kuongeza gharama za uendeshaji.
Chanzo: Nipashe
No comments:
Post a Comment