Mtazamohalisi

Wednesday, December 22, 2010

Nundu Aitaka Mamlaka Ya Usimamizi wa Bandari Kufanya kazi Kiufanisi

SERIKALI imeiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), kwa kushirikiana na Kamati ya Kuboresha huduma bandarini kuhakikisha kwamba kuanzia sasa muda wa uondoshaji wa kontena katika Bandari ya Dar es Salaam unapungua ili TPA iendelee na jukumu lake la kuboresha huduma hiyo na kuleta ufanisi zaidi.

Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu ameitaka TPA kuanza mara moja kujenga na kuimarisha miundombinu ya bandari kwa kuzingatia mpango mkuu wa Mamlaka na kwamba mpango huo ni dira ya kuendeleza na hatimaye kufikiwa kwa lengo la nchi la kuifungua kibiashara ndani na nje ya nchi.

Nundu aliyasema hayo jana Dar es Salaam katika majumuisho ya ziara yake ya siku mbili ya kutembelea TPA ili kuona na kujifunza mambo muhimu ya uendeshaji na uendelezaji wa Bandari ya Dar es Salaam.

Akiongozana na Naibu wake, Dk. Athuman Mfutakamba, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Ephraim Mgawe na viongozi wengine wa bandari, Waziri Nundu alipata pia fursa ya kutembelea baadhi ya kampuni za kuhifadhi mizigo ya bandarini kwa lengo la kufahamu changamoto mbalimbali zinazoikabili mamlaka hiyo.


Alisema wakati ujenzi wa bandari ya Mwambani, Tanga ukiendelea, TPA inununue vifaa vitakavyoongeza ufanisi wa matumizi ya bandari hiyo na kusisitiza shirika lianze mawasiliano na uongozi wa Tanga ili maeneo ya ndani na nje ya bandari yanayotumika kwa shughuli zisizo za kibandari, zichukuliwe na kumilikishwa TPA.

Aidha, alisema mchakato wa kufanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina eneo la Kisarawe kwa ajili ya matumizi ya kuhifadhi mizigo, ufanyike mara moja hata kama ni kwa gharama za serikali na kuongeza kuwa ni vyema hilo likafanyika kabla ya mwaka wa fedha 2011/11 haujamalizika.

Alisisitiza wafanyakazi wa TPA kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na matakwa ya wateja, na kuwa mawasiliano kati ya mamlaka na wateja yawe ya haraka na yenye tija.
Chanzo: Habari Leo

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...