Mtazamohalisi

Friday, December 31, 2010

Kali Za Funga Mwaka

Huko Afrika kusini,kumekuwa na heka heka za mwisho kwa raia wa Zimbabwe kujiandikisha kisheria.
Raia Wazimbabwe atakaye kuwa hajajiandikisha atajikuta anarudishwa nchini Zimbabwe.

Mwezi Aprili ,2009 serikali ya Afrika kusini ilitoa ruhusa kwa Wazimbabwe kuingia nchi hiyo bila kibali kufuatia hali mbaya ya kisiasa na kiuchumi.Kusamehemewa Viza kwa Wazimbabwe,kulikuja kutokana na mazungumzo baina ya nmawaziri wa mambo ya ndani wa Zimbabwe na mwenzake wa Afrika kusini.



Huko Uhispania,wanawake wajawazito wamejikuta wakiharakisha kujifungua ili kuweza kupata posho toka serikalini.
Mabadiliko ya sheria ya mafao ya uzazi yataanza rasmi tarehe mosi 2011,ambapo serikali ya Uhispania imetangaza kusimamisha rasmi utoaji wa posho ya US$ 3000.
Kudidimia uchumi wa Uhispania kumepelekea serikali kusimamisha
posho ya ulezi .

Lengo la utoaji wa posho hiyo,ambayo ilianza rasmi mwaka 2007 lilikuwa ni kuwahamasisha raia wa Uhispania kuongeza vizazi ili kukabiliana tatizo la uhaba wa watu .

"Ili Uhispania kuendelea, inahitaji kuwa familia zenye watoto wengi.Na familia itabidi ihitaji misaada zaidi ili kuweza kuwa na watoto wengi na vyanzo vingi ili kumudu ulezi", Zapatero aliliambia bunge mwaka huo.
Zaidi soma .Aljazeera

Estonia tarehe 1/1/2011 itakuwa mwanachama wa 17 wa muungano wa sarafu wa ulaya,ni nchi ya kwanza toka Muungano wa nchi za soviet kujiunga na umoja wa Ulaya na Nato mwaka 2004.



Brazil -Kwa heri Lula ,karibu Dilma Roussef
Anaanza kazi rasmi tarehe 1/1/2011.
Mwanamke wa kwanza kuwa rais,nchini Brazil

Australia-Sura Tatu Zakaribisha Mwaka Mpya

Kaskazini Ya Australia Yakumbwa na Mafuriko
Ukubwa wa eneo la Kaskazini ni sawa na nchi
ya Ujerumani na Ufaransa kwa pamoja au kwa
nchi kama Marekani ni eneo zima la Texas.
Watu takribani 200000 waokolewa


Kusini Mashariki ya Australia yakubwa na ongezeko kubwa la joto

Hatimaye Mji wa Sydney wafurahia Ujio wa mwaka mpya

Thursday, December 30, 2010

Waziri Akataa Kuuziwa Mkaa Korogwe


Waziri wa Maliasili na Utalii,Ezekiel Maige

Wauza mkaa katika eneo la kijiji cha Chekeleni, wilayani Korogwe mkoani Tanga, walivamia gari la Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, baada ya kusimama ghafla katika eneo hilo na kutaka wamuuzie mkaa wao, wakifikiri ni mteja wa kawaida.


Hata hivyo, ndoto za wafanyabiashara hao ziliyeyuka ghafla, baada ya kubaini kwamba, Waziri Maige si mteja kama walivyofikiria, bali alisimama hapo kutaka kuona kama wanauza mkaa huo kihalali.

Baada ya kugundua kwamba wanayemshawishi anunue mkaa wao ndiye Waziri wa Maliasili na Utalii, wafanyabiashara hao waliokuwa wamepanga maguni ya mkaa pembezoni mwa barabara, waliamua kutimua mbio na kuacha mkaa wao, huku waliobaki katika eneo hilo, wakikana kujihusisha na biashara hiyo.

Waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wa Waziri Maige, walipata fursa ya kuzungumza na baadhi ya wananchi ambapo walidai kuwa wamekuwa wakiuza mkaa kwa Shilingi 7,500 kwa gunia moja.

Wananchi hao walisema kuwa wamekuwa wakiuza mkaa huo kila siku ili waweze kujipatia ridhiki na kwamba baadhi ya maafisa misitu wamekuwa wakiwaomba chochote (rushwa) ili wawaruhusu kuendesha biashara hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa ushuru wa Sh. 1,000.

“Hata hivyo, tunashindwa kuelewa maana mara waje watu wengine na kujiita watu wa TRA, tunawapa ushuru na tunaposhindwa kutoa wanachukua mkaa na kuondoka nao. Mara nyingine wanakuja watu wa halmashauri tunatoa ushuru gunia Sh. 1,000,” alisema mwananchi mmoja na kuoinyesha risiti ya magunia 50.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Athuman Said, alirusha lawama kwa baadhi ya watumishi wa serikali kwamba wao ndio chanzo cha ushuru wa mazao ya misitu kupotea kwa sababu wamekuwa hawatekelezi majukumu yao ipasavyo.

Hata hivyo, mwenyekiti huyo ameishauri serikali kuwabana wachoma mkaa ili waweze kutoa ushuru badala ya kuwabana wafanyabiashara wadogo wadogo tu.

Kwa upande wake, Waziri Maige, aliagiza kwamba maafisa misitu wahakikishe kila anayefanya biashara ya mkaa anatoa ushuru wa Shilingi. 2,000 kwa gunia moja na kwamba wasimamie ipasavyo sheria namba 14 ya mwaka 2004, inayohusu mazao ya misitu.

Waziri Maige aliwataka wananchi kuhakikisha pindi wanaponunua mkaa wapewe risti, ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza na kwamba wakikutwa wakiwa hawana risti watakamatwa kwa mjibu wa sheria.

Waziri Maige aliwaambia wananchi hao kuwa kudai risiti kutasaidia kukusanya mapato ya serikali kwa kiwango kinachotakiwa kwani wakwepaji wa ushuru watakuwa wamedhibitiwa.

“Wananchi wahakikishe pindi wanapouziwa mkaa wapewe risti na muuzaji huyo, maana ukikamtwa huna risiti ni kosa. Na hali hiyo itasaidi kuwabana wakwepaji wa ushuru na hivyo kukusanya mapato ya serikali vizuri,” alisema Waziri Maige, ambaye tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo mwezi uliopita, amekuwa akichukua hatua za kubana wizi wa rasilimali za nchi.
Chanzo: Nipashe

Rais Wa Zamani Wa Israel Apatikana Na Hatia Ya Ubakaji


Rais wa zamani wa Israel,Moshe Katsav

Rais wa zamani wa Israel Moshe Katsav amepatikana leo na hatia ya makosa mawili ya ubakaji, ikiwa ni kilele cha kashfa iliyojitokeza miaka minne iliyopita ambayo ililishangaza taifa hilo la Kiyahudi. Rais huyo wa zamani anakabiliwa sasa na hukumu ya kwenda jela miaka minane.


Wakati mahakama hiyo mjini Tel Aviv ikitoa hukumu hiyo, ambapo pia imemhukumu Katsav kwa madai ya bughdha za kingono, vitendo vinavyovuka mipaka na kuzuwia sheria kuchukua mkondo wake, rais huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 65 ambaye alionekana dhahiri kufadhaika, alikuwa akinong'ona tu, "hapana , hapana".

Hukumu hiyo inakuja baada ya kuendeshwa kesi hiyo ambayo imechukua mwaka mmoja na nusu na kujumuisha madai ambayo ni ya kuhuzunisha, yakimuonesha Katsav kuwa ni mbakaji ambaye mara kwa mara huwasumbua wafanyakazi wanawake katika ofisi yake.

Kiongozi huyo wa zamani wa nchi anashutumiwa kwa kumbaka mara mbili mwanamke mmoja ambaye ametambuliwa kwa jina la "Aleph" wakati akiwa waziri wa utalii, na kuwafanyia usumbufu kingono na kuwabughudhi wanawake wengine wawili wakati akiwa rais. Katsav amesema kuwa hana hatia wakati wote wa uchunguzi wa kesi hiyo ya ubakaji na usumbufu wa kingono.

Awali alikubali makubaliano ya kutoa maelezo yake mahakamani ambayo yangemfanya kukubali madai madogo madogo na kulipa faini ili waendesha mashtaka watupilie mbali madai ya ubakaji, lakini baadaye alibadili msimamo wake, na kufanya makubaliano hayo kuwa batili na kusema anataka kusafisha jina lake mahakamani.

Alilazimika kujiuzulu kama rais , akakabidhi ofisi kwa hasimu wake Shimon Peres. Katsav amewashutumu wahanga wake kwamba wanajaribu kumwendea kinyume na kudai kuwa alikuwa mhanga wa juhudi za kumchafulia jina zinazofanywa na kundi la waendesha mashtaka na vyombo vya habari bila ya yeye kuweza kujitetea. Mwanawe wa kiume Boaz Katsav, baada ya kutolewa hukumu hiyo amesema kuwa baba yake hana hatia.

Tunataka kukata rifaa. Na kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, kila mmoja atatambua kuwa baba yangu , rais wa nane wa taifa la Israel hana hatia.

Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema kuwa ni siku ya masikitiko kwa taifa la Israel na raia wake, lakini ameisifu kesi hiyo kuwa ni ishara ya nguvu za mfumo wa sheria wa nchi hiyo.
Chanzo: Dw

Wednesday, December 29, 2010

Bei Mpya Za umeme Hizi Hapa

SHIRIKA la Umeme nchini (TANESCO) limeainisha gharama mpya kwa watumiaji wa umeme zitakazoanza kutozwa kuanzia mwezi Januari mwakani.

Taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari na Ofisi ya Uhusiano wa Tanessco jijini Dar es Salaam jana ilianisha kuwa gharama hizo mpya zimegawanyika katika makundi matatu kulingana na mahitaji ya matumizi ya umeme.

Makundi hayo ni pamoja na watumiaji wa nishati hiyo kwa matumizi ya majumbani ambapo gharama ya chini kutoka 0-50 kWh/mo utauzwa kwa gharama ya sh 60 badala ya sh 49 ya sasa, tofauti yake ikiwa sh 11.

Kwa upande wa matumizi ya umeme ya kawaida bei ya matumizi kwa gharama za nishati kwa uniti imepanda kutoka sh 129 hadi kufikia Sh 157 ikiwa imeongezeka kwa sh 28.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kadhalika kwa upande wa mahitaji ya juu ya msongo mdogo, gharama za nishati kwa uniti imepanda kutoka sh 85 hadi sh 94 ikiwa imepanda kwa sh 9 zaidi.

Kadhalika mahitaji ya juu ya msongo mkubwa, gharama za nishati kwa uniti ambao ulikuwa ukiuzwa sh 79 sasa utauzwa sh 84 tofauti ikiwa ni sh tano.

Kwa upande wa Shirika la Umeme Zanzibar gharama za nishati kwa uniti kwa gharama mpya ya umeme itakuwa ni sh 83 badala ya sh 75 gharama hizo zikiwa zimepanda kwa sh 8.

Watumiaji ambao wameonekana kuumizwa katika gharama hizi mpya ni wale wa matumizi madogo madogo ya nyumbani na wenye matumizi ya kawaida ambao wamepandishiwa kwa zaidi ya Sh 10.

Kwa muhibu wa taarifa za TANESCO, hatua hiyo ya ongezeko la gharama imefikiwa baada ya gharama hizo kuidhinishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA).

Dk. Slaa Aacha Kilio CCM

USHINDI mwembamba wa Chama cha Mapinduzi (CCM) uliosababisha ruzuku yake kuporomoka, umekiweka chama hicho mahali pabaya baada ya watendaji wake kushindwa kulipana mishahara.

Chama hicho tawala kimefikia hatua ya kushindwa kuwalipa watendaji wake hasa wale wa nchini na kupunguza matumizi baada ya ruzuku yake kushuka kutoka zaidi ya sh bilioni moja hadi sh milioni 800,000 baada ya mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willbrod Slaa kupunguza kura za Rais Jakaya Kikwete kwa kiwango kikubwa.

Habari kutoka ndani ya makao makuu ya CCM, zinasema chama hicho kimepunguza matumizi yake kwa kiasi kikubwa na mara nyingi Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusuf Makamba, amekuwa akiwaambia watendaji hao kwamba hali hiyo inatokana na kupungua kwa ruzuku.

'Sasa hivi hakuna cha vocha wala pesa za posho kama zamani. Tunaambiwa tujitolee, watendaji wa chini waliokuwa wakipelekewa pesa kila mwezi, kama hawawezi kujiendesha, wasitegemee pesa toka makao makuu,' alisema mmoja wa maafisa wa chama hicho, ofisi ndogo ya Lumumba, Dar es Salaam.

Mbali ya kushindwa kulipana mishahara, habari zaidi zinasema watu walioathirika na kimbunga cha Dk. Slaa ni taasisi za CCM ambazo ndizo zilikuwa kinara wa kumpinga Dk. Slaa wakati wa kampeni.

Taasisi hizo zinazomegewa ruzuku kila mwezi mgao wao umepungua na kuna uwezekano wa baadhi yao kufutiwa kabisa.

Baadhi ya taasisi zinazopata ruzuku toka makao makuu ya CCM ni pamoja na kundi la muziki wa dansi, kwaya na maigizo la Tanzania One Theatre (TOT), Radio Uhuru, Kampuni ya Magazeti ya Uhuru na Mzalendo, jumuiya za chama ambazo ni Umoja wa Vijana (UVCCM), Jumuiya ya Wanawake (UWT) na Jumuiya ya Wazee CCM (TAPA).

'Kwanza TOT, magazeti ya Uhuru na Mzalendo na Radio Uhuru, yanaweza kufutiwa kabisa ruzuku maana hakuna maana ya kuwapa ruzuku kama wanapaswa kujiendesha kibiashara na wanapata faida. Mpango huo umeanza kujadiliwa sana pale makao makuu,' alisema mmoja wa makada wa CCM ambaye ni mjumbe wa Halmashauri Kuu.

CCM inapata kiwango sh milioni 800 kutokana na kupata asilimia 60.40 ya kura za urais katika uchaguzi huo, ambazo ni sawa na sh milioni 354 na asilimia 77 ya wabunge (sawa na sh milioni 460) kwa mwezi.

CHADEMA inapata sh milioni 203.6, kwa kupata asilimia 24 ya kura za urais (sawa na sh milioni 146) na asilimia 9.62 ya wabunge (sawa na sh milioni 56) wakati CUF, sasa inapata sh milioni 117.4, kutokana na kupata asilimia 9.80 ya kura za urais (sawa na sh milioni 57.9) na asilimia 10 ya wabunge (sawa na sh milioni 56).

NCCR-Mageuzi inapata ruzuku ya sh milioni 10 kutokana na kupata asilimia 1.08 ya wabunge wakati UDP na TLP vinapata ruzuku ya sh milioni 2.4 kwa kupata asilimia 0.42 ya kura za ubunge kila kimoja.

Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi, ruzuku hiyo hutolewa kwa chama kilichofikisha kuanzia asilimia tano ya kura za urais na kwa uwiano wa wabunge na madiwani, ambao chama kilivuna katika uchaguzi huo.

Ruzuku hiyo ilianza kutolewa Novemba, baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika nchini Oktoba 31, mwaka huu na ule uliofanyika baadaye katika baadhi ya majimbo kukamilisha uchaguzi huo.

Katika uchaguzi mkuu uliopita, Rais Kikwete alipata ushindi mwembamba wa kura milioni tano, sawa na asilimia 61.17, akifuatiwa na Dk. Slaa aliyepata kura 2,271,941, sawa na asilimia 26.34, wakati mgombea wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba aliambulia kura 695,667, sawa na asilimia 8.

Chanzo: Tanzania Daima

Monday, December 27, 2010

Sitta Asubiria Taarifa Rasmi Kuhusu Hoja Ya Mgeja

Vinara wakukemea ufisadi

Waziri wa ushirikiano wa Afrika Mashariki,Spika wa
mstaafu Samuel Sitta akiwa na Mbunge wa SameMashariki
Bi Anna Kilango.

WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amesema amasubiri kwa hamu hoja binafsi iliyoahidiwa kuwasilishwa Halmashauri Kuu ya CCM na Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja,.

Alhamisi iliyopita, Mgeja alimtuhumu Sitta kuwa anaendeleza mgawanyiko ndani ya CCM na kumtaka afute kauli yake kuwa aliondolewa uspika kwa mizengwe, la sivyo atawasilisha hoja binafsi Nec kumtaka athibitishe. 
“Sitta anapaswa kufuta kauli yake kuwa, aliondolewa kwa hila…kikao kilichofanya uamuzi kuhusu nafasi ya uspika ni Kamati Kuu ya CCM. Kwa hiyo anamaanisha wajumbe wa kikao hicho wana hila naye.

Kusema hivyo kutasababisha baadhi ya wanachama kukosa imani na kikao hicho,” alisema Mgeja. 
Akizungumza na gazeti hili juzi, Sitta alisema ingawa hajapata taarifa rasmi kuhusu hoja za Mgeja, anaisubiri kwa hamu.

“Siwezi kuzungumzia kwa kina taarifa ya Mgeja kwa kuwa sijaipata vizuri, lakini ninaisubiri kwa hamu hoja yake hiyo,’’ alisema Sitta ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Tisa.

Wakati Sitta akisita kujibu hoja ya Mgeja, Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango, amemshangaa Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa wa Shinyanga, akisema alichosema hakiwezekani.
Pia, Kilango alipuuza msimamo wa Mgeja akisema hauna mashiko: "Hoja binafsi zinapelekwa bungeni tu, sio kwenye vikao vya chama. Vikaoni zinaletwa ajenda, sasa huoni haya ni maajabu?"

“Huyu mwenyekiti asituvuruge, tunatakiwa kujua chama kinaelekea wapi na tumefikaje hapa,” alisema Kilango na kueleza kuwa anaamini Mgeja katumwa, huku akiongeza:

"Ni bora pia atwambie (Mgeja) ametumwa na nani kwa kuwa anachozungumza ni kudanganya umma."

Kilango ambaye alikuwa akizungumza kwenye mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwake jijini Dar es Salaam jana, alisema anamshangaa mwenyekiti huyo kumwandama Sitta, badala ya kutafakari jinsi alivyopoteza majimbo manne ya ubunge mkoani Shinyanga.

"Huyu anataka tumkate panya mkia halafu aendelee kuishi badala ya kumkata kichwa ili kumaliza tatizo," alisema Kilango akimaanisha kuwa Mgeja anataka kukwepa hoja ya msingi kwa kuanza kuzungumzia mambo yasiyomhusu.

"Namsihi Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, asikubali kuwa na viongozi ndani ya chama ambao wanataka kumkata panya mkia badala ya kumkata shingo ili afe," alisema Kilango.

Alisema hivi sasa CCM inatakiwa kuokoa chama kwa kufanya tathmini kujua chanzo cha wananchi kuwakataa, lakini sio kuzungumzia mambo yasiyo na msingi.

Desemba 19, mwaka huu, Sitta alitoa kauli nyingine inayoweza kutikisa CCM baada ya kueleza kuwa, aliondolewa kwenye kinyang'anyiro cha Spika wa Bunge kutokana na hila za viongozi, ambao walishindwa kuhimili kasi ya utendaji wake kwenye chombo cha kutunga sheria.

Mbunge huyo wa Urambo Mashariki, alijikuta akianguka kwenye kinyang'anyiro hicho baada ya CCM kwa kile kilichoelezwa kuwapa wanawake nafasi ya kuongoza moja ya mihimili ya nchi.
Chanzo: Mwananchi.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...