BARAZA la Vyama vya Soka kwa Nchi za Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), sasa linapita katika kipindi kigumu baada ya Misri kusema itajisikia raha kama litaanzishwa Shirikisho la Soka kwa Nchi za Bonde la Mto Nile.
Kauli hiyo ya Misri ni nyepesi, lakini yenye uzito mkubwa kwani inaweza kupunguza msisimko wa mashindano ya CECAFA na hata kuyaua kabisa na badala yake yale ya nchi za Bonde la Mto Nile kuwa yapo juu, hasa katika suala la zawadi.
Juzi Chama cha Soka cha Misri (EFA) kilitangaza zawadi ya zaidi ya Sh milioni 200 kwa bingwa wa michuano ya soka kwa nchi za Bonde la Mto Nile iliyoanza jana mjini hapa ikishirikisha nchi saba.
Zawadi hiyo ni zaidi ya mara tano ya ile ambayo Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars' ilichukua baada ya kuibuka bingwa wa michuano ya Chalenji mwezi uliopita katika mashindano yaliyofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambapo Stars ilitwaa dola za Marekani 30,000 ambazo ni karibu Sh milioni 43 za Tanzania.
Kutokana na mwitikio mzuri wa nchi zinazoshiriki michuano ya Mto Nile mwaka huu, Misri imesema ipo katika mazungumzo na nchi ambazo bonde hilo lipo, ili kuzishawishi lianzishwe shirikisho hilo ambalo Misri inaamini litakuwa kitovu cha vipaji vya soka Afrika na duniani kwa ujumla.
Rais wa EFA, Samir Zahir alisema juzi kuwa kama nchi zote zitakubaliana kuanzisha shirikisho hilo itakuwa hatua moja kubwa ambayo imepigwa kwa maendeleo ya soka Afrika
Lakini EFA inaona ugumu ulio mbele juu ya kuanzishwa kwa shirikisho hilo kwa vile baadhi ya nchi tayari zipo katika vyama mbalimbali vinavyosimamia soka kwa kanda zao.
Alisema zaidi ya nusu ya nchi zinazoshiriki mashindano hayo ya Bonde la Mto Nile ni wanachama wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), ukiacha Misri na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambayo ni mwalikwa katika michuano hiyo.
Nchi zinazoshiriki michuano hiyo ambazo ni wanachama wa CECAFA ni Tanzania, Kenya, Uganda, Sudan na Burundi na zimekuwa zikishiriki mashindano yanayoandaliwa na baraza hilo karibu kila mwaka.
"Tumepeana changamoto ya namna bora ya kuanzisha shirikisho letu, uwezo wa kufanya hivyo tunao maana dhamira yetu ni kuendeleza soka," alisema.
Nchi nyingine wanachama wa CECAFA ambazo hazijashiriki michuano ya Mto Nile ni Ethiopia, Eritrea, Djibouti, Rwanda na Somalia.
Misri imegharamia usafiri wa kuja Misri na kurudi nyumbani kwa kila timu pamoja na posho za wachezaji na waamuzi, zawadi mbalimbali kwa washindi.
Bingwa wa michuano hiyo atazawadiwa zaidi ya Sh milioni 200 za Tanzania. Pia Rais huyo wa EFA, alieleza kuwa michuano yao ni maalumu kuhamasisha soka na haihusiani na masuala ya kisiasa na kwamba mambo yanayohusiana na siasa ni jukumu la wahusika wenyewe.
"Kwangu mimi ukiniuliza michuano ya soka kwa nchi za Bonde la Mto Nile ina madhumuni gani, nitakwambia ni kuinua soka. Hilo ndilo jibu langu na ndicho ninachokiamini," alisema.
Alieleza kuwa mwaka huu mashindano hayo yamefanyika Misri, hivyo nafasi ipo wazi kwa nchi nyingine ambayo itakuwa tayari kuyaandaa na kwamba Misri itatoa msaada wa karibu zaidi ili kuyafanikisha.
Chanzo: HabariLeo
Wakati huohuo,ufunguzi wa michuano ya soka kwa nchi za bonde la mto mto Nile yaliyofunguliwa jana,kati ya wenyeji Misri na Tanzania yalikuwa kama hivi.
No comments:
Post a Comment