Fatma Maghimbi Ajiunga Na CCM
- Kaongozana na Juma Othman Juma
- Waiaga CUF na kuchukua kadi za CCM
- Waahidi wengi zaidi wanakuja nyuma yao visiwani humo
Wakongwe wawili wa siasa za vyama vingi visiwani Zanzibar Mheshimiwa Fatma Maghimbi na Juma Othman Juma wamerudisha kadi zao za CUF na kuchukua za CCM jana jimboni Kawe jijini Dar es salaam na kuahidi wenzao wengi watafuata nyayo zao kutoka CUF.
Akielezea sababu zake za kurudi CCM, Juma Othman Juma amesema ameguswa kwa kazi kubwa aliyofanya Mheshimiwa Kikwete Tanzania Bara na Visiwani hususan aliporejesha amani na utulivu visiwani Unguja na Pemba kipindi cha uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Alisema tangu historia ya vyama vingi ianze Tanzania, kila wakati wa uchaguzi wananchi wengi wa visiwa vya Unguja na Pemba hulazimika kukimbia visiwani humo kwa kuhofia hali ya kutokuwa na usalama katika kipindi hicho.
"Lakini sasa napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Kikwete kwa kurudisha heshima ya nchi yetu duniani kwani mwaka huu wa kampeni, hakuna hata mmoja aliyehama visiwani humo kukimbia uchaguzi" alimaliza Juma Othman akishangiliwa na umati mkubwa wa wana CCM waliojitokeza kwenye mkutano huo wa kampeni.
Mama Fatma Maghimbi amewahi kuwa waziri kivuli wa Katiba na Sheria ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa kama mbunge wa Chama Cha Wananchi CUF. Naye Juma Othman Juma amewahi kuwa muanzilishi wa Chama Cha Siasa visiwani kabla ya kujiunga na Chama cha Wananchi CUF.
Pichani: Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi Jakaya Mrisho Kikwete akimkaribisha Mama Fatma Magimbi CCM baada ya kurejesha kadi ya CUF kwenye mkutano wa kampeni jimboni Kawe Jijini Dar es salaam.
No comments:
Post a Comment