Mtazamohalisi

Tuesday, October 19, 2010

Kuondoka kwa Maghimbi hakujaiathiri CUF, asema Seif

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amesema kitendo cha aliyekuwa Kiongozi wa Upinzani Bungeni kutoka chama hicho, Fatma Maghimbi, kuhamia CCM ni haki yake kidemokrasia, lakini hakina athari yoyote kwa chama hicho.
Akizungumza na wandishi wa habari mjini Zanzibar jana , alisema CUF hakijapata athari yoyote kisiasa kwa Maghimbi na aliyekuwa Mjumbe wa mkutano Mkuu wa chama hicho, Juma Othman Juma kuhamia CCM.

“Naweza kusema kwamba hatuoni kama tumepata pigo katika hilo, isipokuwa tunamtakia kila la heri katika maisha yake mapya ya kisiasa”, alisema Katibu Mkuu wa CUF.

Alisema kwamba CUF ipo imara na katika kudhihirisha hilo, majimbo yote 18 kisiwani Pemba yataendelea kushikiliwa na chama hicho cha upinzani.

Maghimbi na mwenzake wamekihama chama cha CUF na kuhamia CCM na walikabidhiwa kadi ya CCM na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kawe jijini Dar es Salaam.

Maalim Seif alisema Maghimbi ambaye alikuwa Mbunge wa Chakechake amekihama CUF baada ya kukosa nafasi ya ubunge kufuatia wanachama kumkataa wakati wa kura ya maoni wakati wa mchakato wa kutafuta wagombea wa chama hicho kisiwani Pemba.

“Wapo watu chama kinakuwa kizuri pale wanapokuwa na madaraka wanapokosa chama kinakuwa kibaya, lakini kuondoka kwao hakutaacha pigo lolote kwa CUF, kwasababu hiki ni chama cha wananchi”, alisema Maalim Seif.

Alieleza kwamba tabia ya viongozi wanaokosa vyeo kuhama vyama sio ngeni, kwa vile wapo waliowahi kufanya vitendo kama vya Maghimbi na wamekiacha chama cha CUF kikizidi kuimarika.

Jijini Dar es Salaa, Naibu Mkurugenzi wa Uenezi na Mahusiano CUF, Ashura Mustapha, alisema Maghimbi hana tena mvuto wa kisiasa.

Alisema mwasisi huyo aliamua kukihama chama cha CUF baada ya kuona hana mvuto tena wa kisiasa.

“Ameamua kuhama kwa sababu anaona amepitwa na wakati na wananchi hawamtaki tena,” alisema.

“Maghimbi anadai eti ameamua kuhama CUF kutokana na Upemba kuzidi katika jimbo hilo, lakini tunaamini kuwa wananchi wenyewe ndio walioamua kufanya mabadiliko baada ya kuona hana mvuto tena wa kisiasa, na hata hivyo pia wanaangalia alama za nyakati upo muda wananchi pia wanahitaji mabadiliko,” alisema  Mustapha.

Alisema japokuwa Maghimbi ametumia Demokrasia kuhama chama, lakini pia ameonyesha ni jinsi gani uongozi wake haukua kwa manufaa kwa wananchi.

“Kama kweli Maghimbi hakuwa CUF kwa ajili ya kujinufaisha mwenyewe,asingeweza kuhama kwa kuanguka kipindi kimoja tu,wakati ameongoza kwa miaka kumi,” alisema.

2 comments:

  1. kila mtu ana tafsiri yake katika neno siasa. lakini kwa upande wa wale wasiojua kutumikia watu huona siasa kama ulaji au sehemu ya kujipatia kipato. lakini hiyo ni imani iliyofilisika kabisa.

    watu hao tunao wengi sana katika jamii, si za kiafrika tu bali hata ulaya, marekani na hata asia. siasa imegeuzwa biashara, mtu anahonga pesa nyingi ili awe kiongozi.

    kwa mujibu wa mwanasiasa aliewahi kutokea Afrika Mwl Nyerere alipata kusema kuwa mtu mwadilifu hawezi kukimbilia ikulu. lakini badala yake watu wanahonga ili waingie ikulu, na wapo wanaoita nafasi za uongozi ulaji.

    utasikia mtu ameteuliwa kuwa waziri au katibu mkuu basi ndugu zake wanasema ameula... ameula? nini... nilitegemea wananchi wamuhonge mtu ili agombee ubunge akawatetee bungeni, lakini cha kushangaza watu ndo wanahonga wananchi ili wakawawakilshe bungeni. mmmmhhhh.. nyukira mino.. pukachakaaaaa..

    ReplyDelete
  2. Alama za wanafiki, ni tatu bora muzijue
    Katu nae haaminiki,japo ahadi azitoe
    Pia na hasadikiki, hatumizi maaganoe
    Alama yake ya pili, mnafiki ni muongo
    Maisha hana ukweli, wala mizuri mipango
    Yake usiyakubali, atakukoroga bongo
    Akiaminiwa hukhini, mnafiki ni sifaze
    Hachi na hana dini, hudhulumu hata nduguze
    Usimtie nyumbani, na sirizo simjuze…

    ReplyDelete

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...