Mtazamohalisi

Tuesday, November 9, 2010

Maisha ya Kila Siku Vijijini

Mama na mzigo wa kuni









Dunia ya masikini,yaponzwa na yake njaa
nitumie kuni gani?, nisije pata fadhaa.
sishi kuzichanja kuni, na bado nazisha saa
majasho tele usoni, kama ni ndoo hujaa.
"nishati ipi jamani?, mimi kwangu inafaa".

Kuni za kilimanjaro, nilianza kutumia
kwa njia za uchochoro, kuni zilinifikia
na sasa nina kihoro,theluji ya angamia
limekuwa ni gogoro, na maji yanapotea.
"nishati ipi jamani?, mimi kwangu inafaa"

Nikageukia mkoko, maarufu kule pwani
kwa kuivunja miiko, kumegeuka wangwani
mawimbi sasa kiboko, miji ipo tafrani
ya vunja huko nahuko, na nyumba zipo majini.
"nishati ipi jamani?, mimi kwangu inafaa"

Kwa kuitaka nafuu, naagiza visiwani
kuni za mkarafuu, zilo katwa mashambani
majuto ni mjukuu, nimetiwa mikononi
sheria ndiyo mkuu, najikuta hatiani.
"nishati ipi jamani?, mimi kwangu inafaa"

Nikafanya marejeo, fikira kuzi tembeza 
Amani ni mulekeo, kijiji pale lunguza
misitu waliyo nayo ,kuni tulimaliza
Ajira ya vipepeo, vijana wamepoteza.
"nishati ipi jamani?, mimi kwangu inafaa"

Ikiwa mafuta ya taa, kwa jiko lake la tambi
nalo lataka wasaa,kulimudu ni kivumbi
nahisi bora mkaa, bei yake haigombi
japo kidogo lafaa, kwa sisi watu wa kambi.
"nishati ipi jamani?, mimi kwangu inafaa"

Nishati nzuri umeme, hilo tunali tambua
yapasa mtu uzame, huduma kujipatia
huenda mimi niseme, kheri umeme wa jua
lakini pesa ukame, kuni nime zichagua.
"nishati ipi jamani?, mimi kwangu inafaa"

Mwisho jamani nahisi, jibu muta nipatia
msije nambia gesi, ni endane na dunia
kipato changu halisi, siwezi kufikiria
ikiwa hamto pasi, kuni nitaji katia.
"nishati ipi jamani?, mimi kwangu inafaa"

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...